Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wamachinga wang’oka kwa shingo upande Dar
Wamachinga wang’oka kwa shingo upande Dar
By Habari Tanzania | Published  10/1/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Kulwa Karedia

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo, maarufu kwa jina la wamachinga jijini Dar es Salaam, wameondolewa katika maeneo yaliyopigwa marufuku kwa wao kuendesha biashara, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la miezi sita iliyopita.

Wafanyabiashara hao walitii amri ya serikali ya mkoa kwa kuhama kutoka katika maeneo yaliyopigwa marufuku na kwenda katika maeneo waliyoandaliwa.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, John Lubuva, alisema hadi kufikia jana mchana, zoezi hilo lilikuwa likiendelea vizuri kutokana na wengi wa wafanyabiashara hao kuhama kutoka katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo.

“Tumezunguka maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo na maeneo mengine na kushuhudia wengi wa wafanyabiashara hawa wakiwa wameondoka, hivyo napenda kuwahakikishia kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao yataimarishwa ili wapate huduma zote muhimu za kijamii,” alisema Lubuva.

Mtaa wa Kongo ambao hufurika watu kwa shughuli mbalimbali, jana ulionekana kuwa wazi, huku pilikapilika za kila siku zikiwa zimepungua, hali iliyodhihirisha kuwa agizo la kuwahamisha limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Idadi kubwa ya watu walitegemea kujitokeza kwa matukio ya uvunjifu wa amani kama ilivyokuwa imetangazwa na wamachinga wiki iliyopita, kuwa walikuwa tayari kumwaga damu, lakini hapakuwa na dalili hizo jana.

Mabanda yote katika mtaa huo yalionekana kubomolewa na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa wapita njia kupita bila msongamano mkubwa kama ilivyo kawaida.

Kwa ujumla hali ya jiji ilianza kuonekana katika sura mpya katika maeneo ya Posta ya Zamani, Magomeni, Manzese, Buguruni, Ubungo na Mwenge ambako Tanzania Daima ilitembelea.

Katika hali ambayo ilionekana kuwashangaza wengi, ni pale askari wa Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na polisi walipozuia gulio la Mtaa wa Lumumba ambalo hufanyika kila Jumamosi kwa madai kuwa kwa sasa halihitajiki tena. Gulio hilo lilianzishwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yussuf Makamba.

“Tunasema kuanzia leo (jana) eneo hili halitakuwa tena na soko la kila Jumamosi kama ilivyokuwa imekwisha zoeleka, na badala yake wote mnatakiwa kuhamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili yenu,” alisema mmoja wa askari wa jiji aliyekuwa na kipaza sauti.

Katika eneo la Mchikichini hali ilikuwa tofauti, wafanyabishara walionekana kuwa na kazi moja tu ya kujenga mabanda mapya kwa kasi ya aina yake, huku baadhi yao wakisema wamekubali agizo la serikali.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Adam Shabani aliwataka wafanyabishara wenzake kutii amri ya serikali kwani kufanya hivyo kutawapa nafasi nyingine ya kufikiriwa na serikali wanapopata matatizo.

“Sisi tumekubali kama unavyoona hapa… tunahangaika na kazi moja tu ya ujenzi wa mabanda kwa ajili ya kuendesha biashara zetu ili tuepukane na matatizo tunayopata, pia nawaomba wenzangu wajaribu kutii amri ya serikali,” alisema Shabani.

Katika eneo la Kiwanja cha Sambusha, Kigogo, hali ilikuwa tulivu, huku shughuli za ujenzi wa mabanda zikiendelea bila kasoro zozote.

Eneo la Manzese ambalo hufurika wafanyabishara, lilionekana kuwa tulivu tofauti na siku za nyuma ambako, fujo nyingi zinazohusisha uchomaji moto magurudumu ya magari hufanyika, hali hiyo haikuwepo kabisa, kitendo kilichoashiria kuwa zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Askari wengi wa jiji na polisi, walionekana kurandaranda bila ya kufanyiwa fujo yoyote kutoka kwa wafanyabishara hao, huku wakiwa na virungu, vipande vya mbao kama silaha za kujilinda endapo kungetokea tatizo lolote.

Katika hatua nyingine, wasambazaji wa magazeti jana walishindwa kugawa magazeti katika eneo la Kariakoo kutokana na kuzuiwa na wingi wa askari polisi waliokuwa wametanda katika eneo hilo majira ya saa 11 alfajiri.

Baada ya kuwepo na mabishano makubwa, polisi hao waliamua kuwasiliana na viongozi wa ngazi za juu wa Wilaya ya Ilala kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ndipo polisi hao walipowaruhusu kuendelea na kazi.

“Tumepata shida kubwa mno, polisi waliokuwa wametanda katika eneo hili walituzia kwa muda mrefu kugawa magazeti, lakini najua yote hii ilikuwa kuepuka tatizo la kuwepo kwa wamachinga,” alisema Juma Idd.

Agizo la kuondolewa kwa wamachinga katika maeneo yasiyoruhusiwa lilitolewa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa miezi sita iliyopita, huku akiwataka wavamizi wote walioko katika maeneo yasiyoruhusiwa wawe wameondoka ifikapo jana


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.