WAKATI sekretarieti mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yussuf Makamba ikitimiza siku 100, mambo bado ni magumu kwa chama hicho kunadi fikra mbadala, kuishawishi jamii na makundi ya vijana kuwa kimezaliwa upya.
Miongoni mwa mambo yaliyowahi kushusha heshima ya CCM mbele ya umma na kabla ya kuingia madarakani kwa sekretarieti hiyo, ni matumizi ya rushwa katika mchakato wa kupata mgombea urais na wagombea ubunge, mwaka jana. Mbali na maeneo hayo, rushwa pia ilitawala wakati wa kampeni.
Mambo mengine yaliyobainika kuwachosha wananchi na baadhi ya wanachama wa CCM, ni pamoja na chama hicho kuhusika katika migogoro ya ardhi kwa baadhi ya ofisi zake za matawi kudaiwa kujengwa katika maeneo ya wazi. Katika baadhi ya maeneo, pia CCM imekuwa ikidaiwa kuvamia maeneo ya wazi, ikiweka wapangaji wanaoendesha shughuli za karakana kama gereji.
Kilichotarajiwa na wengi, baada ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa mwenyekiti wa chama hicho na Makamba kuteuliwa Katibu Mkuu ni CCM kuzaliwa upya, upya unaohusisha kutambulishwa kwa fikra mbadala za namna ya kuboresha uwanja wa siasa nchini.
Rais Kikwete alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Juni 25, mwaka huu, na mara baada ya mkutano mkuu wa chama hicho kumchagua, alipendekeza sekretarieti yake, akimteua Makamba kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kinyume cha matarajio ya wengi, CCM iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Benjamin Mkapa na Katibu Mkuu, Philip Mangula, imeendelea kuvaa sura ile ile, ikiwa ni pamoja na kuvumilia harufu ya rushwa na wengine wakisema sektretarieti mpya ni mvinyo wa zamani uliowekwa katika chupa mpya.
Miongoni mwa mambo yanayothibitisha Makamba na sekretarieti yake kupita katika njia aliyotumia Mangula katika kuongoza chama hicho, ni kanuni ya kupora baadhi ya viongozi wa kambi ya upinzani kwa imani kuwa kufanya hivyo ni kudhoofisha upinzani na wakati huo huo kuimarisha CCM.
Bila kutambua hatari inayoweza kukikumba chama hicho kama kitaendeleza kanuni hiyo ya kupora wanasiasa wa upinzani, sekretarieti hiyo imewaamini kwa haraka, kwa kuwapa fursa ya kuongozana na katibu mkuu huyo katika ziara zake mikoani, jambo linaloweza kudhaniwa kuwa ni kutunuku daraja la kwanza la uanachama viongozi hao kutoka upinzani.
Hatari inayoweza kukikumba chama hicho, ni pamoja na baadhi ya wana-CCM kuanza kukariri tafsiri kuwa viongozi kutoka kambi ya upinzani ni kitisho dhidi ya madaraka yao katika chama chao. Huu ni ufa unaopiga hodi mbele ya mlango wa chama hicho.
Kitendo cha sekretarieti hiyo ‘mpya’ kushindwa kutanguliza fikra mbadala zinazoelekeza namna ya kupandisha heshima ya chama hicho mbele ya jamii, na kuboresha mazingira ya uendeshaji wa siasa nchini, ni miongoni mwa mambo ambayo ni mtego dhidi ya sekretarieti hiyo.
Baadhi ya wana-CCM wakosoaji waliozungumza na Tanzania Daima wamesema, walitaraji Makamba na uongozi mpya utajivunia hazina ya vijana waliomo katika chama hicho na kuitumia vema hazina hiyo, huku wageni (kutoka upinzani) wakikaribishwa na kupumzishwa kwa muda maalumu (Probation).
“Katika utaratibu wa chama (CCM), nastahili kuwasilisha maoni yangu katika vikao. Lakini kuhusu hili la siku 100 za huyu jamaa (Makamba) na wenzake, nadhani hakuna jipya. Pengine ni mapema... unajua jambo kubwa lililovuruga heshima ya chama ni hili la rushwa ambalo liliitwa takrima.
“Halafu jingine ni hili la kuchukua watu wa upinzani na kisha bila kufanya tathmini wanapanda daraja na kuwamo katika misafara ya viongozi wakuu,” alisema mwana-CCM mkosoaji kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini kwa madai kuwa hapendi kuvuruga taratibu za chama kutaka malalamiko yawasilishwe katika vikao.
“Kuhusu hawa wanasiasa kutoka upinzani, chama kiwapokee, lakini si kuwaamini moja kwa moja na kusahau wengine waaminifu waliokuwapo awali,” alisema mwana-CCM mwingine aliyewahi kuwa mbunge kwa mihula miwili (si Bunge la sasa).
Wakati ni wazi CCM iliathiriwa kwa kiasi fulani na hatua ya vyombo vya habari kumsusa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Omar Ramadhani Mapuri, Makamba ameonekana kutojifunza kutokana na tukio lake la kuwafukuza waandishi wa habari kutoka katika vyombo binafsi alipokuwa katika ziara yake mkoani Singida.
Pia, Makamba huyo huyo ambaye wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliwahi pia kuingia katika matatizo na vyombo vya habari, pia alijitia matatani mkoani Kilimanjaro wakati alipotoa kauli mbaya dhidi ya wanasiasa wanaohama vyama vya upinzani na kurejea CCM, akidai kwamba wanaganga njaa.
Miongoni mwa magazeti ya kila siku ya Kiswahili yalinukuu kauli yake hiyo aliyoizungumza hadharani, lakini mwenyewe aliibuka na kukanusha kutoa kauli hiyo na hivyo kusababisha malumbano na gazeti hilo ambalo ni miongoni mwa yale yanayoheshimiwa hapa nchini.
Kwa hakika, ndani ya siku 100 za sekretarieti mpya, ubunifu unadhihirika kuwa mtihani mgumu mno, CCM imeshindwa kutumia siku hizo kuonyesha mwelekeo mbadala wa mazingira ya siasa nchini.