Na Shija Felician, Kahama OFISA Masoko wa Kampuni ya G&B Soap Ltd aliyetoa taarifa za uongo katika kituo cha polisi kwamba amevamiwa na majambazi na kuporwa mamilioni ya fedha, mali ya mwajiri wake amehukumiwa kifungo cha miaka 13.
Akisomewa hukumu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Juma Hassan, mshitakiwa, Isdory Tuluka alidaiwa kuwa akiwa mwajiriwa wa kampuni hiyo alitenda kosa hilo Agosti 15,mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa siku ya tukio,Tuluka alikwenda kituo cha polisi na kutoa taarifa ya uongo kwamba alikuwa ameporwa Sh19,950, 000, mali ya mwajiri wake.
Aidha, Mwendesha Mashtaka huyo alidai mahakamani hapo baada ya taarifa hizo, polisi walikwenda kwenye eneo hilo na kukuta hakuna tukio lolote la ujambazi lililotokea hapo na kumtia mbaroni mhusika.
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa Masoko wa Kampuni hiyo, Watambile Chishagimbi baada ya kuwasilisha ushahidi wa maandishi mahakamani hapo ilibainika tayari Tuluka alikuwa ametenda kosa la wizi wa Sh 21 milioni kati ya Machi hadi Agosti mwaka huu.
Mwendesha Mashtaka huyo aliifafanulia mahakama hiyo kuwa Tuluka kuwa alilipwa pesa hizo na wafanyabiashara 12, ikiwa ni mali ya kampuni, lakini alishindwa kuziwakilisha na badala yake alizitumia kwa manufaa yake binafisi, hali iliyomfanya hakimu amtie hatiani kwa makosa mawili ya kuidanganya polisi na kuiba pesa ya mwajiri wake.
Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi kwa mshtakiwa.
Mshtakiwa alikiri makosa yote na kufanya hakimu wa mahakama hiyo amhukumu kutumikia kifungo cha miaka 13