Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Zombe aruka
Zombe aruka
By Habari Tanzania | Published  09/30/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Happiness Katabazi

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Laurian Kalegeya, amesema kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake, imeiva na ipo tayari kusikilizwa.

Jaji Kalegeya aliyekuwa kwenye kiti cha enzi wakati Zombe na wenzake 12 walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu, aliziita habari hizo kuwa ni njema, akazitaka pande zote mbili zisubiri tarehe rasmi ya kuanza kusikilizwa, na kwamba itapangwa katika vikao maalumu vya Mahakama Kuu.

“Washtakiwa msiwe na wasiwasi, nawapeni habari njema kwamba kesi yenu imeiva na hivyo muda wowote kuanzia sasa, itakuwa tarehe ya kuanza kusikiliza kesi yenu, mtaarifiwa kwa njia ya maandishi,” alisema Jaji Kalegeya.

Jana ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa washtakiwa hao kutakiwa kujibu mashtaka yao, kwani awali, taratibu za awali za kesi ziliendeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako hawakutakiwa kujibu lolote, kwa kuwa kesi za mauaji husikilizwa na Mahakama Kuu peke yake.

Na jana, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zombe, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, pamoja na wenzake walikana mashtaka yote waliyosomewa. Wengine katika kesi hiyo namba 26/2006 ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makele, F.5912 Konstebo Noel Leonard, WP.4593 Konstebo Jane Andrew, D.6440 Koplo Nyangelera Moris na D.1406 Koplo Emmanuel Mabula.

Kadhalika, katika kesi hiyo ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini, wazaliwa wa Mahenge, Morogoro, wapo washtakiwa E.6712 Koplo Felic Sandys Cedrick, D.8289 Konstebo Michael Shonza, D.2300 Koplo Abeneth Saro, D.9321 D/C. Rashid Lema, D.4656 D/Koplo Rajab Bakari na D.1367 D/Koplp Festus Gwabisabi.

Mwanasheria wa Serikali, George Masaju, ndiye aliwasomea mashtaka hayo, akisema kwamba, Januari 14, mwaka huu, katika Msitu wa Pande, Mbezi Louis, Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi watu wanne wakidaiwa kuwa ni majambazi. Washitakiwa wote walikana mashtaka na kurejeshwa rumande.

Akisoma maelezo ya kesi, Mwanasheria Masaju alisema kwamba, siku hiyo washtakiwa wote kwa pamoja, walifika eneo la Sinza Palestina, wakawakamata wafanyabiashara watatu waliokuwa na dereva teksi wao, kisha wakawaua, kwa madai kwamba ni majambazi.

Masaju alisema watu hao hawakuwa majambazi, bali walikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuuza madini yao na kulipa ada za shule za watoto wao. Kwamba baadhi ya madini waliyauza kwa mfanyabiashara wa Arusha.

Alisema kwamba, siku hiyo ya Januari 14, watu hao walikuwa na mamilioni ya fedha walizokuwa wamezihifadhi kwenye begi, washtakiwa hao wakachukua begi hilo lenye fedha na bastola iliyokuwa ikimilikiwa kihalali na marehemu Sabinus Chigumbi, maarufu kwa jina la Jongo.

Masaju alisema, askari hao waliwafunga pingu na kwamba raia waishio Sinza Palestina, waliwashuhudia askari hao wakiwa na mitutu ya bunduki, lakini hawakuwashambulia kwa risasi watu hao.

Aliendelea kueleza kwamba, mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu, walikuwa viongozi katika Jeshi la Polisi, walikuwapo kwenye eneo la tukio na walitumia simu zao za mkononi kuwasiliana ili wakawaue watu hao wanne na wawapore fedha na madini.

Masaju alisema kwamba, siku hiyo usiku, washtakiwa waliwachukua watu hao na kuwapeleka kwenye msitu wa Pande, wakawalaza kifudifudi na kuwapiga risasi vichwani, kisha wakachukua maiti na kuzipeleka kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Alisema kuwa, taarifa ya vifo vya watu hao ilithibitishwa na daktari wa MNH, kwamba watu hao waliuawa kwa risasi, kwa kuwa ubongo ulitoka nje, mashavu na uti wa mgongo viliharibiwa sana.

Mwanasheria huyo wa serikali alieleza kuwa, washtakiwa hao walipomaliza kuwaua wafanyabiashara hao na dereva teksi wao, walichukua madini, mamilioni ya fedha, simu za mkononi na bastola, vyote vikiwa ni mali ya marehemu, na walikwenda navyo katika Kituo cha Polisi Urafiki kisha wakagawana fedha hizo.

Aliongeza kuwa, Tume ya Jaji Kipenka Mussa, ilithibitisha marehemu hawakuwa majambazi, na polisi iliamua kufanya uchunguzi na kubaini kuwa washtakiwa wote 13 ndio waliohusika na mauaji ya watu hao.

Wakili Majura Magafu, kwa niaba ya mawakili wenzake wa utetezi, aliieleza mahakama kuwa, kwa mujibu wa maelezo ya mwanasheria huyo wa serikali, upande wao unayakubali mambo matatu.

Mambo hayo ni kuwa; marehemu hawakufa vifo vya kawaida, washitakiwa wote ni polisi, achilia mbali tofauti ya vyeo vyao na kwamba washtakiwa wote walikamatwa kwa mujibu wa mashtaka yanayowakabili.

Hata hivyo, Wakili Magafu alisema kwamba, siku ya tukio Zombe hakwenda msitu wa Pande, kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka. Hoja hiyo ilikubaliwa na Mwanasheria wa Serikali pamoja na mahakama, hivyo Zombe akaondolewa katika hoja inayodai kuwa naye alikuwapo kwenye msitu uliotumika kuwaua wafanyabiashara na dereva wao.

Hata hivyo, Magafu aliiomba mahakama iwape muda ili upande wa utetezi uweze kuandaa mashahidi wake, ambao nao pia watafika mahakamani kutoa ushahidi.

Magafu ambaye alipangwa na serikali kuwatetea washtakiwa wote hao, ameiomba mahakama iwatafutie mawakili wengine kwa ajili ya kutetea baadhi ya washtakiwa, aliosema hawezi kuwatetea, kwa kuwa kuna mgongano wa ushahidi, na kwamba mgongano huo upo kwenye ushahidi wa mshtakiwa namba 11 na 12.

Kwa sasa, Magafu atawatetea washtakiwa namba 5, 6, 7, 9, 10, wakati mshtakiwa namba 4 na 3 watatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Samson Nnko, huku Zombe akitetewa na mawakili Jerome Msemwa na Fatma Karume.

Wakili wa serikali alieleza kuwa kesi hiyo itakuwa na mashahidi 54, miongoni mwao ni Mwandishi wa Habari wa gazeti hili, Happiness Katabazi na kwamba ushahidi umekamilika. Alisema watawasilisha vielelezo mbalimbali, ikiwamo ripoti ya daktari, bunduki, risasi na maganda yake pamoja na alama za vidole vya washtakiwa.

Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kusikiliza kesi hiyo iliyoanza saa 5.30 na kumalizika saa 7 mchana. Hata hivyo mshitakiwa wa tano, Jane Andrew alichelewa kuletwa mahakamani hapo, wakati washtakiwa wenzake walikuwa wameshafika tangu saa tatu asubuhi. Mshtakiwa huyo alifikishwa ndani ya jengo la Mahakama Kuu saa 4.23, akiwa anakimbia mchakamchaka huku akitabasamu.

Wote wanashtakiwa kwa kuwaua wafanyabaishara wanne, Ephrahim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo’, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu ambaye alikuwa ni dereva wa teksi iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao katika shughuli zao.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by an unknown user)
    Rating
    hao polisi wanyongwe!!!!!!!!! majambazi makubwa hayo!! unawaua watu wasiokua na hatia wenye familia zao zinazowategemea!! hii kesi inauma sana hao polisi lazima haki ipatikane sio mambo ya kuyayushana tu mara kesi imeisha!!
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.