Kuhamishiwa kwa kituo cha mabasi toka Mwenge kwenda Makumbusho katika Manispaa ya Kinondoni kumeongeza idadi ya wafanyabiashara wapya katika soko la Makumbusho lililokuwa likidoda kwa muda mrefu ambapo sasa wafanyabiashara kibao wanaendesha shughuli zao hapo.
Awali soko hilo lilikuwa na wafanyabiashara 66 pekee ambapo sasa, hadi kufikia jana, tayari idadi hiyo ilishapaa na kufikia wafanyabiashara 450.
Ongezeko hilo limekuja katika kipindi cha wiki sita kati ya nane zilizotangazwa na Manispaa ya Kinondoni kuwa zitatosha kukamilisha ujenzi wa kituo cha mabasi Mwenge.
Makamu Mwenyekiti wa soko la Makumbusho, Bw. Hassan Omary amesema kuwa ongezeko hilo linaweza kuwa changamoto mpya kwa Manispaa yao ya Kinondoni kuhakikisha kuwa kituo hicho hakihamishwi tena.
Alisema kati ya wafanyabiashara hao, 115 wapo nje ya soko kuzunguka stendi ya mabasi, 15 ni Mama Lishe na wote waliosalia wanauza bidhaa ndogondogo zikiwemo nyanya, matunda, mbogamboga na bidhaa nyinginezo zisizokauka katika soko lolote lile la maana kama lao.
Akasema Bw. Omary kuwa hivi sasa, ni meza chache zinazododa ambapo kati ya 220 walizo nazo na mabanda 70 yanayozunguka soko, tayari kuna wafanyabiashara kibao waliojitwalia nafasi na kuendelea na shughuli zao za kujiingizia vipato halali.
Hata hivyo, Bw.Omary akasema kuwa ongezeko hilo lingesaidia kuongeza pato la Manispaa kupitia kodi ya ushuru, lakini msimamo wa sasa wa serikali kutowatoza ushuru wafanyabiashara hao umekwamisha upatikanaji wa fedha hizo.
Hata hivyo, Bw. Omary alisema kuwa nafasi sokoni kwake hapo bado zipo bwerere na kusema kuwa kama utaratibu wa sasa wa kusisitiza uwepo wa matumizi ya kituo hicho cha mabasi, nafasi zote zingejaa.