WAKATI uzalishaji wa zao la pamba nchini ukiongezeka kutoka marobota 196,000 msimu wa 1999\2000 hadi takriban marobota 700,000 mwaka jana, wakulima walichuma hasara ya shilingi Bilioni 31.4 kufuatia wanunuzi matajiri kupeleka pamba chafu katika soko.
Hii ni sawa na kusema, wakulima walilima sana kwa takriban muongo mmoja,lakini badala ya kulipwa kulingana na bei ya soko, wakajikuta wanapunjwa shilingi 31,350,337,637/= kufuatia soko helela liitwalo ‘huria’. Matajiri walioshiba, walikusanya pamba chafu na kuiuza.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Joseph Mungai,alisema Aprili 20 mwaka huu, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta Ndogo ya Pamba, uliofanyika jijini Mwanza, kwamba tatizo hilo la aibu likiendelea kufumbiwa macho,litawaletea wakulima hasara na Taifa kwa ujumla.
“Uhalifu huo usipodhibitiwa, pamba yetu itaendea kununuliwa kwa bei hafifu na kuwekewa ‘karantini’ya uchafu katika soko la kimataifa”, Waziri Mungai alisema. Wakulima wa pamba hawauzi zao hilo moja kwa moja katika masoko ya kimataifa.Huuza pamba yao kwa wanunuzi wenye leseni, kulingana na sheria na taratibu zilizopo. Kama kuna wanunuzi wasio na leseni, au Wamachinga, huo ni udhaifu wa sheria na usimamizi. Mkulima hausiki kwa namna yoyote na tatizo.
Hivyo, kila msimu wa mauzo unapofika,wakulima huuza pamba yao kwa wanunuzi. Pamba hiyo hununuliwa baada ya wahusika kuridhika kwamba inao ubora unaotakiwa katika soko.
Lakini, miezi kadhaa baadaye, wakulima wamekuwa wakiarifiwa kuwa wanalazimika kukatwa malipo yao halali kutokana na pamba chafu kukataliwa katika soko la Kimataifa!
Kulingana na hali hiyo, Waziri Mungai anasema: “Haifai kabisa kuruhusu watu wachache (kumbe wanaruhusiwa) kuendelea kuchafua pamba yetu, na pia kuendelea kuchafua jina jema la nchi yetu katika soko la Dunia.
Kuendelea kufanya hivyo, ni kuhujumu uchumi wa Taifa letu…ni kuwahujumu wakulima wetu”.alisema Mungai. Ameiagiza Bodi ya Pamba kusimamia na kuratibu juhudi za kurejesha usafi wa pamba yetu. Pamba ya Tanzania ilikuwa safi; yenye ubora katika soko la Dunia, kabla ya kuhujumiwa na wajanja kwa tamaa ya utajiri. Nani “aliondoa” ubora wa pamba ya Tanzania na kuwakosesha wakulima bei halali?
Kulingana na kauli ya Mungai mwenyewe kwamba, ‘watu wachache’( wakulima siyo wachache) kuruhusiwa kuendelea kuchafua pamba yetu, Huharibu jina zuri la nchi yetu na kuwahujumu wakulima… wenye dhamana ya usimamizi wa pamba hawataokoka katika lawama, ingawa hawahukubali kuambiwa ukweli.
Pamba huuzwa kulingana na madaraja: A(safi) na B(fifi). Tangu enzi za Ushirika wakulima walikuwa wakitenga pamba yao katika madaraja hayo wakati msimu unapofika. Soko holela (huria) lilipoanza, baadhi ya wanunuzi waliofumbiwa macho na mamlaka husika wakanunua pamba chafu, safi na fifi iliyonyunyiziwa maji, mchanga takataka, kemikali nk. ili kuongezea uzito!
Laiti mkulima angejua kwamba siku moja atapunjwa bei halali, asingekubali ujinga huu.
Mungai amesema tatizo hilo lilifumbiwa macho (bila shaka na mamlaka zinazohusika) kwa sababu wanazojua wao, ili mkulima aendelee kuwa ‘daraja’ la kuendea neema ya utajiri!
Mifumo, kanuni,na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa masoko zilitibuliwa. Baadhi ya wanunuzi na wenye vinu vya kuchambulia pamba wakaanza kulumbana na Bodi ya Pamba;juu ya nani ni chimbuko la tatizo hilo. Kwa kuwa si kusudi hapa kutafuta mchawi katika sakata hilo, makala hii itaachana na jambo hilo.
Hata hivyo, mkulima wa pamba hajalipwa asilimia 55 hadi 75 ya bei ya soko la Dunia. Hulipwa kiduchu;na kutozwa ushuru,kodi, na tozo nyingine za kinyonyaji za Bodi yenyewe,michango ya Elimu na kinachoitwa, Mfuko wa Kuendeleza zao la Pamba (CDF) wakati wakulima hawajaendelea hata siku moja na kundokana na jembe la mkono na nyumba za nyasi!!
Mwaka huu, pamba imeuzwa kwa bei kubwa hadi sh.400 si kwa sababu nyingine yoyote, ila kiangazi za cha mwaka jana. Kama wanabisha, na waseme kuwa pamba ilipanda bei kwa sababu gani.
Haijafahamika kama pamba huendelezwa toka mahali gani hadi wapi,wakati wakulima wakipata hasara ya mabilioni kutokana na sakata la pamba chafu.Ukiacha mirija mingi iliyowekwa na vigogo katika zao hili, ili kumkamua mkulima hadi tone la mwisho la damu yake, hakuna anayejali mafanikio ya mkulima!
Kila msimu, mirija elfu hubuniwa na kumwekea mkulima huyu shingoni: Mara mchango wa Mwenge, Elimu, Mfuko wa CDF, Pembejeo, sijui jimbo na kila makamuzi! Ili mradi wajanja waweke mirija shingoni mwa mkulima huyu, na kumnyonya damu na jasho hadi tone la mwisho.
Kwa bahati serikali imeondoa ushuru wa Bodi na wa Elimu, ili kuwawezasha wakulima kupata ongezeko la bei, angalau ifike shilingi 270 ambayo ni sawa na asilimia 68.7 ya soko la kimataifa. Hatua hii ya serikali “Ya Kasi Mpya” imekuja kukiwa na madai yaliyotolewa katika kikao kilichopita, cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, kwamba fedha wanazokamuliwa wakulima wa pamba huishia kujenga vitambi vya vigogo!
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Momose Cheyo,alikabidhi Bungeni ushahidi wa madai ya fedha hizi za wakulima wa pamba kujenga vitambi ‘vya wanene’badala ya kumuinua mkulima kutoka shimo la ufukara,dhiki nyingi na njaa ya miongo mingi tangu nchi ipate uhuru.
Kwa kuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta, tayari ameweka utaratibu wa kuweka ushahidi mezani kabla ya kutoa hoja, makala hii inaiweka kando hoja ya fedha hizi kubugiwa na wajanja, yasijekunikuta yaliyomkuta Cheyo na Mbunge wa Tarime, Zakayo Chacha Wangwe…kuwasilisha ushahidi mezani!!
Nihoji basi ikiwa Mfuko wa kuendeleza zao la Pamba (CDF) una manufaa ya moja kwa moja kwa mkulima wa zao hili kijijini. Anawezeshwa nini? Anaendelezwaje? Amesaidiwaje kudhulumiwa malipo na wamachinga wa soko?
Ameachana na jembe la mkono kwa kukopeshwa trekta? Au anawezeshwa pembejeo kiasi gani ili azalishe japo kilo 720 kwa ekari, kama siyo porojo na ujanja-ujanja? Kwa kuwa Awamu hii “Kasi Mpya”imedhamiria kuboresha mazingira ya kilimo, ili kuleta maendeleo kwa kila Mtanzania,waliouza mbegu mbovu zikakataa kuota miaka michache iliyopita, hawana budi kulipa fidia!
Mbegu hizo ziliondolewa maganda ya juu kwa kemikali (acid delinted seeds)bila kufuata taaluma. Matokeo yake, zilipouzwa kwa wakulima, hazikuota. Hivyo wakulima walikoseshwa mavuno ya msimu mzima, kufuatia maelfu ya ekari kutoota.
Kwa kuwa kitendo hicho cha uzembe wa wahusika kilihujumu uchumi wa mkulima, Bodi ya Pamba nchini iliwaamuru wahusika kumlipa mkulima fidia ya mbegu katika msimu uliofuata, badala ya fedha taslimu!
Mkulima alisababishiwa hasara, baada ya kununua ‘bidhaa’ zisizo na ubora. Badala ya wauzaji wa bidhaa hizo “feki” kukamatwa na kufunguliwa mashitaka mahakamani kwa hujuma hiyo, wakaamuriwa kumfidia mkulima mbegu nyingine katika msimu wa kilimo uliofuata!
Hakuna aliyefikiria hasara ya gharama za kilimo, mategemeo ya faida ambayo mkulima angepata, wala maisha yake kwa mwaka ambao alisababishiwa kutovuna mazao, kukosa fedha za matumizi, za matibabu, chakula, malazi, mavazi, au hata faida.
Maeneo yaliyoathiriwa na tatizo hilo ni pamoja na maeneo ya wilaya za Musoma vijijini, Bunda, Sengerema, na Geita. Kwa upande mwingine, mkulima wa Tanzania bado havuni kwa tija. Huvuna wastani wa kilo 300 hadi 400 kwa ekari. Ili kumwezesha kuvuna kilo 800 hadi 1000 kwa kila ekari, serikali ya Kasi Mpya inapaswa kuachana na vibwagizo vya “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe!” Badala yake,iwawezeshe wakulima kulima kwa tija. Nguvu bila maarifa katika zama hizi ni ujinga. Pia serikali hii ya Kasi Mpya, inapaswa kuondoa mirija shingoni mwa wakulima wa zao hili.
Mirija hii iliyowekwa na ‘wajanja’;tena wenye shibe, dhidi ya wakulima masikini wenye njaa,ikiondoka badala yake wakulima wakawezesha pembejeo kwa bei nafuu, kama siyo kupewa ruzuku,pamba , dhahabu nyeupe, itajenga vijiji vya wakulima 500,000 nchini, na kurahisisha utekelezaji wa ahadi ya Maisha bora kwa kila Mtanzania.
Ni kwa hali hii wakulima wataacha kuwa ‘ng’ombe wa maziwa’ kwa wajanja hawa wasiojua kiangazi wala masika, lakini huvuna jasho la wakulima kila msimu. Pamba ya Tanzania ilikuwa ikipendwa katika soko la dunia tofauti na ilivyo sasa. Ilikuwa na sifa sawa na ile ya Australia, Brazil, Zimbabwe na California. Ilipata bei ya upendeleo (Premium) wa kati ya senti nne na sita za Dola ya Marekani, kwa kila ratili(sawa na kati ya shilingi 35 na 53 kwa kilo).
Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka jana,pamba ya Tanzania imedorora kwa sababu ya visingizio tele: Kama kilimo hususan cha pamba na mazao mengine ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, kitaachwaje kunyong’onyezwa na wazembe? Kitaachwaje kuliwa na mafisadi? Kitakosaje usimamizi wa dhati? Uti wa mgongo wa kisayansi, utaachwaje kuchezewa-chezewa na dumuzi, wakati unabeba kila kitu ,ikiwemo mishipa ya fahamu ya Taifa zima?
Kwa kuwa Awamu hii imedhamiria kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania (wakiwemo wakulima wa Pamba) ni mategemeo kuwa hatutaridhika na wingi wa takwimu za uzalishaji wa marobota ya pamba, badala yake serikali itajivunia hali bora za wakulima zitakazooekana kwa macho matupu, bila darubini za takwimu!
Takwimu hizi huwanufaisha vigogo na matajiri wachache zaidi, wakati wakulima wa Mahenge, Bunda, Minjigu, Saragana, Bugoji, Suguti , Wanyere, Mwibara,Sikonge, Magu, Sengerema, Geita na Shinyanga, wakiwa hoi kwa njaa kila mwaka.
Lengo liwe kumwezesha mkulima kuishi kulingana na jasho lake, kuliko kuwawezesha wajumbe wa mkutano wa sekta ya pamba kula, kunywa na kulala vizuri na kuwezeshwa kutembelea ‘mashangingi’ wakati wakulima wakiwa hawana pembejeo, mbolea, na hata nyumba za kuishi, kwa sababu ya ujanja-ujanja!
Kama maisha ya mkulima wa pamba, “dhahabu nyeupe”, hayatabadilika ili kuachana na usafiri wa punda, anapopeleka mgonjwa wake hospitalini,maendeleo ni kitu gani kwake? Kama atalima daima bila tija, ataepukaje kuwa ng’ombe wa maziwa, kwa kujifunga mkwiji kwa njaa, kwa mwaka mzima, lakini mavuno yakaja kuliwa na wenye vitambi, wanaoshinda kwenye viyoyozi? Hivi pamba hulimwa na wenye njaa na kuvunwa na wenye shibe, eeh?
Mwandishi wa makala haya hupatikana kwa simu namba 0754 838066 au barua pepe: omybabu@yahoo.com