HATUA za kumpata mhandisi mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja la mto Kilombero zinakaribia kukamilika baada ya kampuni tano za washauri hao kujadiliwa katika bodi ya tenda ya mkoa.
Meneja wa Wakala wa barabara mkoani Morogoro Injinia Charles Madinda alisema ofisini kwake jana kwamba hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu aliahidi kujenga daraja katika mto huo.
Alisema mradi wa ujenzi wa daraja hilo unagharamiwa na Serikali ya Tanzania ambapo jumla ya sh. milioni 50 zilitengwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa awali. Hata hivyo alisema kati ya fedha hizo tayari serikali imetoa fedha taslim sh. milioni 30.
Mto Kilombero unatenganisha wilaya za Kilombero na Ulanga ambapo umekuwa ni chanzo cha matatizo makubwa ya usafiri hasa wakati wa masika. Hivi sasa wakazi wa wilaya hizo hutumia pantoni kwa ajili ya kuvuka.
Alisema mkoa umeweka mikakati ya ujenzi wa madaraja katika maeneo mbalimbali ambapo madaraja mengi ni ya zamani na yanahitaji matengenezo sambamba na barabara kadhaa.
Alisema hata hivyo tatizo kubwa kwa ajili ya utengenezaji wa barabara na madaraja linasababishwa na upatikanaji wa pesa kwa wakati mwafanya na ufinyu wa bajeti katika kukidhi matengenezo ya barabra hasa zile za changarawe na udongo ambazo zinaharibika mara kwa mara kutokana na uzito wa magari na mvua wakati wa masika.
Madinda alisema kuwa upungufu wa wafanyakazi nao ni tatizo kutokana na ongezeko kubwa la kazi na katika kuhakikisha kuwa kazi zinasimamiwa kwa karibu zaidi.
Akizungumzia kuhusu matatizo ya nje Madinda alisema kumekuwepo na uwezo mdogo wa makandarasi wazalendo hali inayosababisha kuchelewa kukamilika kwa mikataba sambamba na upungufu wa mitambo ya kufanyia kazi.
Alisema utaratibu mgumu katika mabenki wa kupata dhamana kwa ajili ya taratibu za kimikataba nao umekuwa ni tatizo na hivyo kupendekeza kuwa benki watafute utaratibu mzuri utakarahisisha upatikanaji wa dhamana.
Akizungumzia utunzaji wa barabara kwa kutumia mizani ambayo huwazuia wasafirishaji kubeba mizigo mikubwa, Madinda alisema tatizo kubwa ni udanganyifu unaofanywa na wasafirishaji ambao wamekuwa wakipunguza mizigo wafikapo katika mizani.
Alisema hata hivyo udhibiti huo umesaidia kwa kiasi kikubwa ambapo sasa magari yamepunguza kubeba mizigo mikubwa kutoka asilimia 10 hadi 5.9.