WANAFUNZI wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Ufundi ya Moshi (Moshi Technical), wanatuhumiwa kuchoma moto maktaba ya shule hiyo na kusabisha uharibifu mkubwa wa vitabu.
Tukio hilo limetokea kati ya saa 10 na saa 11 alifajiri ya jana, baada ya mwanafunzi mmoja kuona wingu zito la moshi uliotanda ndani na nje ya maktaba hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo, mkuu wa shule hiyo, Isaac Malisa amekiri kuwa moto huo umewashwa na wanafunzi.
Alidai kuwa maktaba hiyo ilikuwa iteketezwe kabisa kwani kulikuwa na jaribio kubwa la kuiteketeza kutokana na kukutwa kwa chupa za plasiki zikiwa na mafuta ya taa huku zikiwa zimewekewa tambi.
Alitaja vitu vilivyoteketea kuwa ni meza, simu ya mezani pamoja na idadi kubwa ya vitabu huku thamani yake ikiwa bado haijajulikana.
Mwalimu huyo amedai kwamba, moto huo ulizimwa kwa ushirikiano wa baadhi ya wanafunzi na walimu na kulaani kitendo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Venance Tossi alikiri kutokea kwa tukio hilo, na kuongeza kuwa, moto huo ulizimwa kabla ya kuleta madhara makubwa. Hata hivyo hakuna mwanafunzi aliyekamatwa kuhusu na tukio hilo.