MTUMISHI wa Quran, Sheikh Yahya Hussein, amewageuzia kibao Waislamu, akisema kwamba wenyewe ndio walioamua kufutwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Sheikh huyo ambaye pia ni mtaalamu wa nyota, aliwaambia waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana kwamba, Waislamu walifanya hivyo kwa itikadi za dini.
Alisema Waislamu ndio walioishawishi serikali kupeleka muswada wa kufutwa kwa mahakama hiyo bungeni mwaka 1963 kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Sheria, Sheikh Amri Abeid Kaluta, aliyekuwa kiongozi wa Madhehebu ya Kadini.
Kauli hiyo ya Sheikh Yahya inakuja wakati kukiwa na mjadala mzito juu ya kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi, kukiwa na makundi mawili, moja likipinga kwa kusema ni kinyume cha katiba na jingine likisema ni haki ya kidini ya Waislamu.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limeshaeleza msimamo wake wa kutaka kurejeshwa mahakama hiyo, wakati maaskofu kadhaa wameeleza kuipinga, wakisema italeta mpasuko nchini.
Wanasiasa nao wamegawanyika katika makundi mawili, baadhi wakishikilia kwamba lazima ianzishwe, kwa sababu ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Sheikh Yahya alikuwa amewaita waandishi wa habari, akisema alilenga kuzungumzia iwapo Mahakama ya Kadhi bado inahitajika au imepitwa na wakati, na kwa nini makanisa yalianzisha mahakama hizo, yakazisimamia na kuziendeleza hadi mwaka 1962 na jinsi Waislamu walivyoamua zifutwe bungeni.
“Ukadhi hapa nchini ulivunjwa na Waislamu wenyewe kwa itikadi za kidini. Waziri wa Sheria wa Tanganyika, hayati Sheikh Amri Abeid Kaluta, Mwislamu ambaye wakati huo alikuwa kiongozi mkuu wa Madhehebu ya Kadini, ndiye aliyeishawishi serikali kupeleka muswada bungeni kufuta Mahakama ya Kadhi.
“Muswada wa kufanya mabadiliko hayo uliokuwa ukiitwa ‘Magistrate Court Bill 1963, uliwasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha tisa cha Bunge kilichofanyika Desemba 3 hadi 5, 1965.
“Muswada huu ulikuwa kimya na haukugusia chochote kuhusiana na Mahakama ya Kadhi au mahakama nyingine za aina hiyo, ili kuendelea kusimamia sheria za dini ya Kiislamu kwa kiwango mahsusi,” alisema Sheikh Yahya.
Alisema Wakristo wa madhehebu ya Kikatoliki, Kilutheri na Kianglikana, ndio walioanzisha na kuendeleza mahakama hiyo, kwa hoja zilizokuwapo wakati huo kuwa serikali ilikuwa za dini yao.
Aliwashangaa Wakristo kwa kuonyesha wasiwasi, baada ya kutaka kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi wakati tangu utawala wa Wakristo wa Kireno, Wajerumani na Waingereza waliziendeleza mahakama hizo.
Alisema mahakama za Kislamu ziliundwa kwa tangazo la serikali namba 8 la 1925 lililotamka bayana kuwa masuala au mashauri yote ya ndoa, mirathi, talaka na mengine yanayohusika na Sheria za Kiislamu, yahukumiwe katika Mahakama ya Kadhi au liwali kwa kutegemea matakwa ya wahusika.
Mnajimu huyo, alisema Mahakama ya Kadhi inahitajika mara tatu zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa uhuru. Alisema umuhimu wa mahakama hiyo unatokana na kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa, ambako Waislamu waliogawanyika katika vyama hivyo laziwa wawe na kadhi wa kuwaunganisha.
Alitaja sababu nyingine ya umuhimu wa kuwapo mahakama hiyo, kuwa ni kuibuka kwa jumuiya nyingi za kidini baada ya BAKWATA, zinazodai ubora wa jumuiya zao na kupinga uongozi wa jumuiya nyingine.
Alisema sababu nyingine ni kwamba, misikiti kupewa usajili kamili wa udhamini na Wizara ya Sheria ambayo maimamu wao na wadhamini wanajitambua kuwa ni viongozi wa Waislamu.