WAZIRI wa Maji, Stephen Wasira, ameuagiza uongozi wa Bohari Kuu ya Maji kuanza haraka mchakato wa kuibadilisha na kuwa wakala wa serikali ili kupambana na ushindani wa soko huria.
Akizungumza na wafanyakazi wa bohari hiyo juzi, wakati wa ziara yake mkoani Dar es Salaam, Waziri Wasira alisema hatua hiyo itaisadia bodi hiyo kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea serikali kama ilivyo sasa.
“Nawaomba kuanzia sasa, mkuregenzi na wenzako muanze mchakato wa kuibadilisha bodi na kuwa wakala wa serikali ili muweze kuendesha biashara yenu vizuri na kuacha kutegemea serikali, na pia kupambana na biashara katika soko huria la sasa,” alisema Waziri Wasira.
Katika bodi hiyo, alishuhudia mlundikano wa vipuri ambavyo hutumika katika shughuli za ufungaji wa mabomba vilivyokosa soko kwa muda mrefu.
Alisema bodi hiyo imekuwa ikikosa soko baada ya kuwepo kwa sekta binafsi ambazo zimefanikiwa kupata soko kubwa la kuuza vipuri kuliko bodi hiyo.
Akiwa katika Chuo cha Maji cha Rwegarulila, Wasira amekitaka chuo hicho kuhakikisha kinatoa elimu bora, kwani sasa Tanzania imeonekana kuwa na uhaba wa wahandisi wa maji.
“Sasa hivi Tanzania ina uhaba mkubwa wa wahandisi wa maji, hivyo hakikisheni mnatoa elimu iliyo bora ili kuondokana na tatizo hili ambalo sasa linaonekana kuwa kero,” alisema Wasira.
Katika ziara hiyo, Wasira alitembelea Wakala wa Kuchimba Visima na Mabwawa. Alisikitishwa na hali ya uchakavu wa mitambo inayotumika katika uchimbaji wa visima.
“Mitambo hii inatia huruma, kuna mitambo ina miaka 35 hadi 70, ingekuwa binadamu, nina hakika angekuwa tayari amefariki, lakini serikali tayari imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununua mitambo hii,” alisema Wasira