JIJI la Arusha ni miongoni mwa maeneo yenye masikini na matajiri wengi.
Kwa anayepita Arusha mjini, hawezi kujua ukubwa wa umasikini katika jiji hilo, hadi atakapotembea viunga vyake.
Ili kuupunguza, na hatimaye kuutokomeza umasikini, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, zinapaswa kufanya mambo fulani.
Miongoni mwa mambo hayo, ni kusimamia suala la ulipaji kodi. Jiji la Arusha, linakabiliwa na uzembe mkubwa wa ukusanyaji kodi.
Sheria zipo, lakini zinavunjwa. Sheria zimetungwa ili zitumike kujenga jamii yenye maendeleo, lakini si kwamba sheria zipo ili zivunjwe.
Inasikitisha kuona kuwa, Arusha inakabiliwa na janga kubwa la ukwepaji kodi kwenye biashara ya magari.
Wakati jijini Dar es Salaam suala la teksi bubu limebaki kuwa la maeneo ya nje kabisa ya jiji, Arusha mambo si hivyo.
Watu wananunua magari madogo na kuyatumia kama teksi katikati ya jiji ilhali viongozi, yaani polisi na Halmashauri ya Jiji ikishuhudia bila kuchukua hatua zozote.
Stendi Kuu ya Mabasi, na katika vituo vyote vya mabasi, kumejaa teksi bubu. Wahusika hawaogopi, hawachukuliwi sheria. Hawahamasishwi kusajili teksi hizo ili zifanye kazi kwa mujibu wa sheria.
Tunaweza kusema mengi, lakini kwa ufupi ni kwamba Arusha ina teksi bubu nyingi pengine kuliko mji wowote katika jamhuri hii.
Je, kwa ukwepaji kodi huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatawezekana? Wapi ambako maisha bora yaliwezekana kwa watu kukwepa kodi au kuendesha biashara bila kulipa kodi? Je, viongozi wa Arusha wamelala wapi?
Inakuwaje viongozi hawa ambao wako karibu na Ngurdoto kunakoendeshwa semina elekezi, wawe wa kwanza kulala usingizi wa pono huku sheria zikivunjwa?
U-Geneva wa Arusha aliouzungumza Rais Clinton wa Marekani ni upi? Ni huu wa teksi bubu kuzagaa kila mahali bila kukamatwa?
Tuna ushahidi wa wazi kuwa wamiliki wengi wa teksi hizi ni polisi, maofisa wa TRA, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na wengine ambao wanajua si rahisi kuguswa na mkono wa dola.
Changamoto tunayoitoa kwa uongozi wa Arusha, ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafuata sheria halali. Sheria ya kulipa kodi, ni sheria halali inayopaswa kutekelezwa na kila mmoja.
Nchi hii haitaendelea kama sheria zitabaki kuwa kwa ajili ya kundi fulani tu la wanyonge. Bila kulipa kodi, maisha bora kwa Mtanzania utakuwa ni msemo unaochusha. Viongozi watekeleze wajibu wao. Wahakikishe kodi zinalipwa. Arusha inatia aibu kwa wingi wa teksi bubu