Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Waziri asema ndege za serikali Tanzania zimezeeka
http://www.habaritanzania.com/articles/1122/1/Waziri-asema-ndege-za-serikali-Tanzania-zimezeeka
By Ramadhan Semtawa
Published on 09/27/2006
 
WAZIRI wa Miundombinu, Basil Mramba, amesema karibu ndege zote za serikali zimezeeka na zinapaswa kununuliwa nyingine mpya.

Na Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Miundombinu, Basil Mramba, amesema karibu ndege zote za serikali zimezeeka na zinapaswa kununuliwa nyingine mpya.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hili jijini Dar es Salaam jana, Mramba alisema kama ni kuzingatia sheria za kimataifa za usafiri wa anga, ndege hizo za serikali zisingeruhusiwa kuruka angani.

Mramba alisema sababu zinazofanya kuwepo haja ya kununua ndege hizo, ambazo ziko kwa Wakala wa Ndege za Serikali ni pamoja na kwamba ndege hizo aina ya Fokker zina zaidi ya miaka ya 30 tangu ziliponunuliwa, hivyo ni hatari kwa usalama wa abiria na kuongezeka gharama uendeshaji kutokana na kuzeeka.

Hata hivyo, waziri Mramba alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali haijatenga bajeti kwa ajili ya kununua ndege nyingine mpya, kwani bado yanaangaliwa maeneo mengine ya kipaumbele.

Mramba alizitaja ndege hizo ambazo zinamilikiwa na serikali kupitia wakala wake, kuwa ni Fokker 50 na Fokker 28 Jet na nyingine ndogo ambayo alisema hata hivyo, haitumiki sana.

"Ndege za serikali zimezeeka, kama ni sheria, basi ndege zilizozidi miaka 30 katika nchi nyingine haziruhusiwi kuruka angani," alisisitiza Mramba.

Hata hivyo, Mramba alikiri kwamba gharama za kununua ndege moja ni kubwa ambapo huanzia wastani wa dola za Marekani 25 hadi 40 milioni.

Kuhusu taarifa kwamba, kuna kampuni ya ndege kutoka Brazil ambayo iko nchini kutaka kuiuzia serikali ndege, alisema hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamekwishafanyika kati ya serikali na kampuni hiyo.

Mramba alisema anafahamu kwa kusikia, kwamba kuna kampuni hiyo ambayo iko nchini na kuongeza kuwa, kama itahitaji mazungumzo na serikali haitakuwa tatizo