Na Mussa Juma, Arusha
CHAMA cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Arusha (AREMA), kimeipinga filamu ya Watumwa wa Vito kwa madai kuwa kwa sasa hakuna watoto wanaotumikishwa katika machimbo ya tanzanite Mererani.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Isaya Latema, amesema madai ya watoto kutumikishwa katika migodi hiyo si ya kweli kama inavyoonekana kwenye picha hiyo, kwani tangu 1998 Serikali iliweka taratibu za kuzuia utumikishwaji watoto na kutekelezwa.
"Tunapenda kuujulisha umma wa Watanzania na Ulimwengu mzima kwamba madai kuhusu utumikishwaji wa watoto katika migodi ya Tanzanite Mererani si ya kweli, " inasema taarifa ya AREMA.
Iliongeza kusema kuwa, Serikali baada ya kutangaza eneo la Mererani kuwa maalum na kutoa vitambulisho kwa wachimbaji wote , hakuna mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 anayeruhusiwa kufanya shughuli yoyote kwenye migodi hiyo.
Chama hicho, kimedai kuwa, filamu hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Habari la IRIN imetengenezwa katika eneo maarufu la Machekecho ambalo serikali ililifunga kutokana na kutokuwa na udhibiti na kusababisha vifo vya wachimbaji.
"Tumefuatilia filamu hiyo... tumebaini haikupigwa migodini bali imepigwa katika eneo la machekecho na vijana wengi wanaohojiwa si wachimbaji kama wanavyodai, " iliongeza kudai taarifa hiyo na kuongeza kuwa lengo la filamu hiyo ni kuporomosha biashara ya madini ya Tanzanite Mererani.
Chama hicho kimeiomba serikali kukanusha filamu hiyo kwa madai kuwa, ina lengo la kuwadhoofisha wachimbaji wadogo ambao hawana nguvu za kujitangaza kimataifa ili wauze madini yao.
Filamu hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni nchini Marekani inaonyesha utumikishwaji wa watoto wenye umri chini ya miaka 14 katika migodi hiyo. Hata hivyo bado Wizara ya Nishati na Madini haijatoa kauli juu ya filamu hiyo