Na Mwandishi Maalum
RAIS Jakaya Kikwete ameonya kwamba duniani inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukabiliana na tofauti za kidini kuliko wakati mwingine wowote.
Amesema,"kwa nchi kama yetu Tanzania, lazima tujiepushe kuchanganya dini na siasa kwa gharama yoyote ile," kwa sababu kunaweza kulitumbukiza taifa katika matatizo makubwa bila sababu za msingi.
Alikuwa anatoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Boston, nchini Marekani uliohusu Menejimenti ya tofuati za Kidini katika Mazingira ya Kidemokrasi, uzoefu wa Tanzania.
Rais Kikwete ametoa mhadhara huo wakati hapa nchini kuna fukuto la viongozi wa dini ya Kiislam wakitaka kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi huku viongozi wa upande wa dini ya Kikristo wakipnga hoja hiyo kwa nguvu.
"Hatuna chaguo jingine zaidi ya kufanyakazi kwa bidii kuhimiza na kuendesha mijadala kati ya dini na dini na kuhimiza kuvumiliana," alisema huku akishangiliwa na wanafunzi na wageni waalikwa akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.
Rais Kikwete alifafanua kwamba, mambo yanayohusu dini na imani mara zote yamekuwa na mwelekeo wa kuwagawa watu kati ya misingi ya 'wao na sisi' na mbaya zaidi katika misingi ya wale wanaoamini na wasioamini.
Alionya kwamba kama migawanyiko hiyo haitaeleweka na kuchukuliwa vizuri inaweza kuwa mikali zaidi.
"Dunia inayo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Thomas Aquinas mwanatheolojia na mwanafalsa wa Kitaliano ambaye alisema ni lazima tuwapende wote, ambao tunaunagana mkono na mawazo yao na wale ambao tunapingana mawazo yao, kwa sababu, wote wametoka jasho katika kuutafuta ukweli na wote wametusaidia sisi katika kuutafuta ukweli huo," alisisitiza Rais Kikwete.
Akisisitiza athari za kutokuwepo uvumilivu wa kidini, alisema kutokuwepo kwa uvumilivu kati ya dini na dini kunachangiwa zaidi na kutofahamu vema misingi ya dini nyingine inasimama katika nini.
Rais Kikwete alisema wakati mwingine mitizamo tofuati husababisha tofauti hasa pale inapotokea kwamba, dini yao ina kandamizwa.
Alisema Tanzania imeweza kuwa na misingi mizuri ya watu wa dini mbalimbali kuheshimiana na kuishi kwa kila mtu kuzingatia imani yake, kunatokana pia na serikali ambayo haina dini isipokuwa watu wake ndiyo wenye dini.
Katika mhadahra huo ambao uliandaliwa na Taasisi ya Utafiti inayoshughulika na viongozi wastaafu wa Afrika, taasisi inayoongozwa na aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania, Charles Stith, Rais Kikwete alibainisha kwamba Tanzania imeweza kuwa na misingi mizuri ya amani iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Alifafanua kwamba, uhuru wa kuhubiri dini lakini bila kutuoa mwanya huo kukashifu dini ya mingine ni jambo jingine ambalo limeweka na kujenga umoja wa kitaifa na maelewano.
Rais Kikwete hatua kali za kisheria huchukuliwa kwa watu wenye kutoa kashfa kwa dini nyingine, kuharibu mali ya dini au kueneza vitendo vyenye kuchochea mitafuruku ya kidini.
Alisema mijadala ya kidini kati ya madhehebu mbalimbali ni moja ya chachu ya kuendelea kuwapo kwa maelewano na mardhiano miongoni mwa waumini wa madhehebu tofauti.