WATU 16 wamekufa na wengine 41 wamejeruhiwa vibaya katika ajali ya basi la Kampuni ya Champion.
Basi hilo lenye namba T 198 AAG, lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, lilipinduka katika daraja la Bamba lililopo eneo la Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani.
Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema ilitokea saa 4 asubuhi; wakati dereva wake alipokuwa akilipita lori lenye shehena ya mafuta.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ephraem Mrema, alisema abiria 15 katika basi hilo, walikufa papo hapo, ilhali mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Christina, alikata roho akiwa katika matibabu katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha.
Mrema alisema majeruhi watatu, Mathayo Anthony; Salum Nyorika (35), mkazi wa Kondoa; na mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana, walipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Majeruhi waliolazwa Tumbi ni Samwel Chisui, Seif Abdallah (22), Ramadhani Mtawa (20), Keneth Njovu (29), Said Juma (20), Ezekiel Magayo (31), Masanja Shimba (28), Kamba Seme (32), Majid Issa (24), Mohamed Abeid (49), Twaha Omar (40), Deus Chichi (38) na Bangwa Bernard (25).
Wengine ni Azira Lubolubo (mtoto), Huruma Msemwa (43), Bruno Stanford (3), Nassor Juma (5), Said Kasim (23), Mbwana Tangalala, Maneno Hamisi (30), Abdul Sharif (20), Yusuf Salum (25), Jonathan Chungu (53), Jakson Christopher, Peruz Ramadhani (30) na mtoto wa mwaka mmoja ambaye hakutambuliwa jina.
Mrema aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Mwazani Rajab (32), Marry Mayalima (45), Ester Mnyanyika (26), Rose John (1.5), Janeth Majuto (4), Sophia Tupa (34), Mwasiti Salum (15), Stella Mwakabenga, Chiku Juma (43), Zamzam Salum (24), Asha Juma (8), Emiliana Jakson (30) na Lucia Salehe (8).
Kwa mujibu wa Mrema, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo. Alisema katika harakati za kutaka kulipita lori la mafuta, ghafla dereva aliona gari jingine mbele, na katika juhudi za kulikwepa, ndipo basi lilipotumbukia darajani na kusababisha maafa hayo.
Hali jana ilikuwa ya simanzi kubwa, huku vilio vikitawala eneo la ajali na hospitalini Tumbi.
Hali ilikuwa mbaya, kwani baadhi ya vilivyowasilishwa hospitalini ni vichwa, mikono, miguu na viungo vya ndani vilivyokuwa vimetenganishwa na viwiliwili.
Bodi la basi liling’oka, kiasi cha kuvifanya viti viwe wazi.
Baadhi ya majeruhi waliwapongeza polisi kwa kusaidia kudhibiti uporaji ambao tayari ulianza kufanywa na baadhi ya wananchi “waliolaanika”.
Polisi walimshikilia Zena Omary (25), mkazi wa Kongowe, kwa tuhuma za kuiba nguo na mikate ya wahanga wa ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma, alifika eneo la ajali, huku akitokwa machozi.
Pamoja na kuwapongeza polisi na wananchi waliojitokeza kuwasaidia majeruhi, Dk. Ishengoma, alituma salamu za rambirambi kwa wafiwa wote, na akawapa pole majeruhi.
Viongozi mbalimbali, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mizengo Pinda; na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Gilbert Dololo; walifika eneo la ajali, na baadaye hospitalini Tumbi.
Mkoa wa Pwani umekuwa miongoni mwa mikoa inayoandamwa kwa ajali.
Hivi karubuni, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lilianzisha utaratibu kwa polisi kusindikiza mabasi yaendayo na kutoka mikoani, lakini haifahamiki ilikuwaje jana basi hilo likawa katika mwendo kasi.
Mwaka 1999, basi la Air Msae liliua watu 25; mwaka 1995 basi la Sai Baba liliua watu 19; mwaka jana basi la JVC nalo liliua watu 16.