Na Furaha Omary
MAHAKAMA Kuu imeelezwa jinsi Wakili wa kujitegemea Eliutherius Kapinga alivyouawa kwa 'kupigwa roba' shingoni na kumaliziwa kuuawa kwa kupigwa nondo kichwani.
Maelezo hayo yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani na mshitakiwa wa kwanza, ambayo yalitolewa mahakamani jana kama kielelezo.
Katika maelezo hayo ya mshitakiwa wa kwanza, Zacharia Mahushi au Ngosha, alisema baada ya Kapinga kuingia ndani Ramadhani Amri ambaye ni mshitakiwa wa pili, alimkaba, akamvunja shingo na kumtupia sebuleni na yeye pamoja na Sadick walimpiga na nondo.
Shahidi Shuruti Tua (48), alieleza hayo wakati akisoma maelezo ambayo aliyachukua kutoka kwa mshitakiwa Mahushi ambaye alikuwa ni mtunza bustani nyumbani kwa Kapinga.
Shuruti ambaye ni Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, ambaye awali alikuwa Hakimu katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, alidai hayo mbele ya Jaji Juxon Mlay wa Mahakama Kuu Tanzania, alipokuwa akitoa ushahidi wake.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Arafa Msafiri, shahidi alidai kuwa Juni 14, mwaka 2002 alikuwa katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, ambapo aliletwa mshitakiwa Mahushi na askari kwa ajili ya kuchukua maelezo yake kuhusu tuhuma za mauaji.
Shahidi alidai alijitambulisha kwa mshitakiwa na kumuambia yupo huru kutoa maelezo, pia alimuambia hayo maelezo atakayoyatoa yatatumika kama kielelezo mahakamani atakaposhitakiwa na Jamhuri.
Alidai Mahushi alikubali kutoa maelezo hayo kwa ridhaa yake ambayo alisomewa na kuridhika nayo na wote wawili wakatia saini.
Shuruti alidai kuwa alimuuliza mshitakiwa jina lake, umri, mahali anapoishi na kama wakati alipokamatwa alipigwa au alipata misukosuko.
Alidai kuwa Mahushi alimuambia kuwa wakati alipokamatwa alipigwa teke la tumbo na askari na kupata maumivu hata hivyo wakati anafikishwa kwake maumivu yalipungua.
Katika maelezo hayo ambayo Shuruti alimkariri (Mahushi), alisema alikamatwa Juni 10, mwaka 2002, saa 10 usiku, Vingunguti katika nyumba ya kulala wageni ya PM akiwa na mkewe.
Mahushi alisema alikutana na Ally (mshitakiwa wa nne), ambaye alimuuliza kuwa anasikia anafanya kazi nyumbani kwa Kapinga ambapo alimjibu ndio, ndipo alipomwambia kuwa kuna dili la kuuza gari na yeye atapatiwa sh.milioni mbili.
Alidai walikubaliana na kwenda nyumbani kwa Ramadhani, ambaye ni mshitakiwa wa pili wakaongozana hadi kwa Sadick ambapo walikuja watu watatu akiwemo askari akiwa na sare za Jeshi mwenye cheo cha Koplo na kumwambia kuwa wanataka gari la Kapinga.
Mahushi alidai siku ya tukio, baada ya kuingia ndani ya nyumba ya Kapinga wakiwa na wenzake wanne, waliwafunga kamba wafanyakazi wa ndani, Salome na Joyce na kudai kuwa Ramadhani aliingia chumbani kwa Kapinga na kuchukua pochi ambalo alichukua sh.milioni mbili na yeye akaambulia sh.laki saba. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa tena leo.