ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, na wenzake 11, kwa mara ya kwanza, keshokutwa watasimamishwa kizimbani, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kusomewa mashitaka ya mauaji ya wananchi wanne.
Kwa mujibu wa hati, kesi hiyo imepewa namba 26/2006. Itatajwa katika mahakama ya wazi saa tatu asubuhi.
Watuhumiwa watasomewa mashitaka yanayowakabili kwa mara ya kwanza. Watatakiwa kujibu mashitaka hayo kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai. Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kesi hiyo itatajwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jaji Laurian Karegeya. Tanzania Daima jana haikufanikiwa kupata majina ya mawakili wa pande zote.
Kabla shauri hilo halijafikishwa Mahakama Kuu, lilikuwa likisikilizwa na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sivangilwa Mwangesi.
Agosti 11, mwaka huu, alikamilisha taratibu na hatimaye kupelekwa Mahakama Kuu.
Pamoja na Zombe ambaye ndiye mshitakiwa namba moja, wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Urafiki, Christopher Bageni; Ahmed Makele; Noel Leonard; Jane Andrew; na Koplo Nyangelela Morris.
Wengine ni Koplo Emmanuel Mabula; E.6712 Felix Sandys Cedrick; Koplo Michael; D.2300 Abeneth; DC Rashid Mahmoud Lema; D/CL. Rajab Hamis Bakari; na Koplo Festus Philipo Bwabishabi.
Wote wanaendelea kushikiliwa katika mahabusu ya Ukonga, Dar es Salaam.
Inadaiwa kwamba, Januari 14, mwaka huu, maeneo ya Pande kwenye Msitu wa Mbezi Louis, waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro, na dereva teksi mmoja.
Waliouawa ni Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi au Jongo, Ephaim Sabinus Chigumbi; na dereva teksi Juma Ndugu.
Washitakiwa walikuwa wakitetewa na mawakili Jerome Msemwa na Fatuma Karume.
Wakati huo huo, kesho kesi ya mauaji yaliyotokea Chang’ombe Village, Dar es Salaam, itatajwa mbele ya Jaji Laurian Kalegeya.
Jamhuri inamshitaki Ayoub Bahati na wenzake wanne kwa mauaji hayo. Mtu mmoja alikufa kwa kufukiwa kwenye kifusi baada ya jengo la Chang’ombe Village, kuanguka kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ujenzi usiozingatia viwango.