JENGO lililokuwa likitumika kama Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Zanzibar, limeuzwa kinyemela na kugeuzwa ghala la kuhifadhia saruji.
Jengo hilo lililopo Mtaa wa Kwa Abass Hussein mjini Zanzibar, limeuzwa hivi karibuni na sasa linatumika kwa shughuli za kibiashara. Askari waliokuwa wakilinda ofisi hizo, wameondoka.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambayo ni wakala wa NEC, Masauni Yussuf Masauni, alithibitisha kuwapo kwa taarifa za kuuzwa kwa jengo hilo.
“Hata sisi tunasikia taarifa hizo, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuzungumzia vizuri suala hilo, kwa vile sisi tunavyofahamu jengo hilo walipewa Tume ya Taifa kuendeshea shughuli zao za uchaguzi,” alisema.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa jengo hilo limechukuliwa na kigogo mmoja serikalini (jina linahifadhiwa) ambaye ana historia ndefu na siasa za visiwani.
Habari zilizopatikana zimeeleza kwamba Diwani wa eneo hilo, Khamis Amour, amejitahidi kufuatilia sakata hilo, ikiwa ni pamoja na kukutana na Kaimu Mkurugenzi wa ZEC, Idrisa Jecha.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba ofisa huyo naye alishangazwa na hatua hiyo kwa vile alidai ofisi yao haina taarifa yoyote kuhusu ukarabati wa ofisi hiyo unaoendelea pamoja na kugeuzwa ghala la saruji.
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Omar Makungu, alipoulizwa na Tanzania Daima, alisema kwamba wao wanafahamu kuwa jengo hilo hadi sasa ni lao kwa vile walipewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Sisi tunafahamu jengo hili bado ni letu na hatuna taarifa yoyote kama limeuzwa, na ofisi zetu bado zitaendelea kuwapo hapo hapo,” alisema Makungu, ambaye pia ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Mratibu wa ZEC, Salum Juma Mgunya, alisema hana taarifa ya kuuzwa jengo hilo, ingawa ameshuhudia likifanyiwa matengenezo makubwa.
Jengo hilo zamani lilikuwa likimilikiwa na Shirika la Biashara na Viwanda, kama kituo cha ushirika wa viwanda vidogo vidogo, ambalo lilishindwa kujiendesha kibiashara.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na wimbi kubwa la majengo ya Serikali ya Zanzibar kuchukuliwa na baadhi ya wakubwa au familia za wakubwa bila ya kutangazwa zabuni.