SIRI ya bomoa bomoa Jangwani, Dar es Salaam, hatimaye imefahamika, baada ya kuwapo habari kwamba sehemu ya eneo hilo maarufu, imeuzwa kwa matajiri wanne.
Habari zilizopatikana mwishoni mwa wiki zilisema eneo hilo limeuzwa tangu mwaka 2004.
Miongoni mwa wanaohusishwa na uuzaji huo ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwingine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, wakati huo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Kuuzwa kwa eneo hilo kumethibitishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Jangwani, Kata ya Charambe, Mohammed Bendera.
Alisema viongozi hao wawili ni miongoni mwa viongozi kadhaa waliotia saini uuzaji huo katika kikao kilichofanyika Novemba 26, 2004.
Bendera alisema alipinga kwa nguvu zote uuzaji huo, na akaenda mahakamani kufungua kesi.
“Nilipingana na suala la uuzwaji wa eneo hilo, na kulipeleka katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi na hadi sasa kesi hiyo haijatolewa uamuzi wowote, ingawa serikali imeamua kuchukua sheria mkononi,” alisema.
Bendera aliwataja matajiri hao, lakini kwa kuwa hawajapatikana kuthibitisha au kukanusha, Tanzania Daima kwa sasa inaendelea kuhifadhi majina yao.
Lakini miongoni mwao ni mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi, kampuni ya ujenzi ya kigeni, na raia kutoka Afrika Kusini.
Bendera alisema kimsingi, viwanja hivyo viliuzwa mwaka 1990, na kwamba kilichofanyika mwaka 2004 ilikuwa ni kubariki uuzaji huo.
Alisema wananchi wanaondolewa eneo hilo kwa sababu serikali inataka kuwasafishia njia hao waliouziwa.
“Serikali inatumia kigezo cha mafuriko katika eneo hili kuwaondoa wananchi, lakini ukweli ni kwamba wanataka wahame ili wawapishe wenye pesa, waweze kujenga kwenye viwanja vyao.
“Ikumbukuwe kuwa viwanja hivyo wamepewa matajiri hao kwa kivuli cha uwekezaji, eti watawekeza,” alisema Bendera.
Bendera alisema kuwa si kweli kwamba sehemu walipojenga wanachi hao hapafai kwa makazi na kama hapafai, iweje tajiri mmoja apewe kiwanja eneo hilo chenye namba 1033/1?
Alisema viwanja hivyo vilimilikishwa kwa baadhi ya wakazi tangu mwaka 1974 kwa kufuata agizo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye pia alitoa msaada wa visima sita kwa wakazi wa hapo.
Alisema atahakikisha anapambana hadi upeo wake, kwa kuwatetea wananchi, na kwamba kama ni kuwaondoa, serikali inapaswa kuwatafutia wananchi hao mahali pengine watakakojenga, na pia walipwe fidia.
Bendera alisema kuwa kitendo kilichofanywa na serikali ni kuvunja haki za binadamu na utawala bora.
Alisema serikali inapaswa kusubiri kwanza uamuzi wa mahakama ambao unasubiriwa kwa hamu.
Pia alihoji kuwa inakuwaje Sheria ya Ardhi, kifungu namba 4 (1), ivunjwe kwa ardhi ya Tanzania kumilikishwa wageni?
Nyumba zaidi ya 70 zimeshabomolewa katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Bendera alisema alikataa rushwa kubwa aliyopewa na viongozi kadhaa wa serikali ili afute kesi mahakamani.
Katika rushwa hiyo, alisema alipewa mifuko 400 ya saruji, mabati na vifaa kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba ya kisasa.
“Nilikataa, nikasema siwezi kuwasaliti wananchi wangu,” alisema.