Na Maura Mwingira, Washington DC
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar jana imetia saini mkataba wa makubaliano (MoU) na Chuo Kikuu cha Kitaifa cha South Caroline ambapo Chuo hicho kitaipata Serikali ya Mapinduzi Zanzibar msaada wa vitabu vya kiada vyenye thamani ya dola za Marekani milioni tatu.
Mkataba huo wa makubaliano ulitiwa saini kwa pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Haroun Ali Suleiman kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha South Caroline, Dk. Andrew Hugine na Naibu Mtawala wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani, (USAID), katika hafla fupi iliyofanyika jana katika ofisi za Makao Makuu ya USAID, yaliyopo Washington DC.
Msaada wa vitabu hivyo unatokana na mpango maalum ambao Rais George Bush ameuandaa wenye thamani ya dola za Marekani milioni 600 wa kusaidia baadhi ya nchi za Afrika wa kuinua na kuendelea sekta za elimu kwa kutoa mafunzo kwa walimu pamoja na vitabu.
Zanzibar ilianza kupokea msaada huo wa vitabu kufuatia ziara aliyoifanya Mke wa Rais wa Marekani, Laura Bush ambaye baada ya kutembelea madrasa zinazotoa elimu kwa watoto wa masomo ya awali aliamua kutoa msaada wa vitabu katika mpango ambao utadumu kwa miaka miwili.
Akizungumza kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo, Rais wa Chuo Kikuu cha Caroline, Dk. Hugine, alisema chuo chake kimeamua kutoa msaada wa vitabu hivyo kuitikia wito wa Rais Bush wa kusaidia ukuaji wa sekta ya elimu katika bara la Afrika, na pia kuunga mkono huhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu katika visiwa hivyo.
Pamoja na kutoa vitabu hivyo, Rais huyo wa Chuo Kikuu cha South Caroline pia aliahidi kuwa chuo chake kitakuwa kinatoa nafasi moja kila mwaka kwa mwanafunzi atakayefanya vizuri mitihani yake kutoka Visiwani humo kwenda kusoma katika chuo kikuu hicho.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, ambaye ni miongoni mwa mawaziri wanaofuatana na Rais Jakaya Kikwete katika ziara hii ya Marekani.Pamoja na kukishukuru Chuo Kikuu cha South Caroline kupitia USAID kwa msaada huo, alisema kuwa, kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao, tangu ulipoanza mpango huo wa kutoa vitabu vya ziada kwa wanafunzi wa shule mbalimbali visiwani humo.
Akaongeza kuwa wanafunzi wasichana wamekuwa wakiongoza katika kufanya vizuri katikamitihani hiyo, na kuahidi kuwa udhamini wa kwanza itakayotoka katika Chuo hicho cha South Caroline ataitoa kwa mwanafunzi wa kike atakayekuwa amefanya vizuri zaidi.
Alisema kuwa msada huo wa vitabu pia umechangia katika uandikishwaji wa watoto wanaoanza shule za msingi na ambao umefika asilimia 100 wa awali wa miaka miwili ambapo serikali ya Marekani kupitia USAID ilitoa msaada wa vitabu kwa madrasa za mjini Zanzibar.
Naye Kaimu Mtawala wa USAID, Lloyd Dierson, alisema kuwa baada ya mafanikio makubwa yaliyopatika kutokana na mpango wa awali wa kusambaza vitabu huko Visiwani Zanzibar, serikali ya Marekani ilikuwa inaangalia pia uwezekano wa kuusambaza msaada huo Tanzania Bara.
Alisema kuwa Shirika lake litatuma wataalamu wake Julai, mwaka huku kuja nchini Tanzania kwa lengo la kufanya upembuzi yakinifu ili utoaji wa vitabu hivyo ufanyike kwa Tanzania Bara pia.
Hadi kufikia Septemba 2005, mpango huo wa kusambaza vitabu na vifaa mbalimbali vya mafunzo na utoaji wa mafunzo kwa walimu (AEI) ulikuwa umetoa nafasi za masomo 120,000 katika nchi 40 za Afrika, ulisambaza vitabu zaidi ya milioni 2.1 na vifaa vingine vya kufundishia na umetoa mafunzo kwa walimu wapya wapatao 60,000 katika nchi 15 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.