Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Nduna: Mwanamke aliyepania kuibadilisha Kilombero
http://www.habaritanzania.com/articles/11/1/Nduna:-Mwanamke-aliyepania-kuibadilisha-Kilombero
By Habari Tanzania
Published on 10/7/2005
 
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), wiki iliyopita kilifanya mafunzo kwa wanawake wanasiasa wanaowania ubunge kupitia majimboni.

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), wiki iliyopita kilifanya mafunzo kwa wanawake wanasiasa wanaowania ubunge kupitia majimboni.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yalianza Alhamisi na kumalizika Jumamosi. Yaliwakutanisha wanawake 75 wa vyama mbalimbali.

Miongoni mwa wanawake hao, alikuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kilombero, mkoani Morogoro kwa tikiti ya CHADEMA, Bi Nduna Kiwanga.

Katika mafunzo hayo, miongoni mwa mambo waliyojifunza ni namna ya kuhutubia katika mikutano ya hadhara, ili hotuba zao ziwe na habari za kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Pia katika warsha hiyo, wanawake hao walikuwa wakiigiza kwa ukweli namna wanavyotoa hotuba za kujinadi katika majimbo yao, na kama kulikuwa na makosa, walikuwa wakikosoana, aliyetoa hotuba nzuri alipongezwa.

Bi Nduna aliposimama kutoa hotuba yake, alisifiwa kwa vile alivyoweza kuwasisimua wenzake ambao wakati huo, waligeuka kuwa ni wapiga kura wake.

Bi Nduna alijenga hoja, kuanisha matatizo yanayolikabili jimbo analowania kuwa mbunge, na kueleza ni kwa namna gani atakapofanikiwa kuwa mbunge ataweza kuyatatua ili Kilombero ipate maendeleo.

"Tujiulieze, Kilombero tumemkosea nini Mungu? Hivi matatizo yote hayo ni amri ya Mungu? Au yanatengenezwa na wanadamu!" Anahoji Bi Nduna huku wenzake wakimsikiliza kwa makini.

Anasema ni ukweli usiopingika kuwa, Mwenyezi Mungu anawapenda sana wananchi wa jimbo hilo ndiyo maana amewaweka katika wilaya yenye ardhi, hali ya hewa na mazingira mazuri ikilinganishwa na baadhi ya wilaya nchini.

"Kama ni ardhi tunayo kubwa, yenye rutuba inayostawisha mazao kadhaa wa kadha, hali ya hewa nzuri, maji ya kutosha yanayotiririka milimani, mito haihesabiki, sana sana hufurika na kuleta maafa," anabainisha na kupigiwa kofi na wenzake na kuendelea:

"Ndugu wananchi, nakumbusha rasilimali zilizopo ndani ya wilaya yetu kama hifadhi ya Uzidungwa, misitu ya mbao, mtambo wa umeme wa Kidatu, Kiwanda cha Sukari Kilombero, mradi wa mitiki, vyote nilivyovitaja na nisivyovitaja ni rasilimali zetu sote na mapato yanayotokana na vyote hivyo yanufaishe wana Kilombero wote," anasema.

Katika mahojiano na mwandishi wa habari, anasema, wakazi wa Kilombero takribani 377,000, hawawezi kumiliki rasilimali hizo mmoja mmoja, ila wanahitaji wa kuzisimamia kwa haki wote wanufaike.

Hivyo basi, anasema hawana budi kupata madiwani, wabunge na rais, ambao wataelewa maana ya dhamana waliyopewa na kutenda haki ili mgawanyo wa rasilimali ufanyike pasipo ubadhirifu na ufisadi.

"Haiwezekani tuchague diwani, mbunge na rais wa chama kilekile, mafisadi wale wale, wakipora uchumi wetu, kwa nguvu mpya, kasi mpya na ari mpya," anasema Bi Nduna.

"Wao huja kwa kutoa takrima na fedha, khanga, fulana, kofia na ahadi kemkemu inapofika wakati wa uchaguzi ili warudi madarakani, nasi tukabweteka na kuwakubali ati watakuwa wasimamizi wazuri, hao hatari! Hawafai na tusiwape kura zetu," anasisitiza.

Pasipo kumtaja mtu wala chama, anasema kwa kuwa hawatendi haki, watafanya jitihada za kurudisha gharama zao walizozitumia, na kukosa muda wa kuwahudumia na kuwaongoza wananchi.

"Matokeo ya haya yote tutaburuzwa, kudharauliwa na kubezwa, kushurutishwa kwa ushuru holela ambao utakusanywa kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya na tusijue la kufanya kwani wao ndio watakaokuwa wameshika mpini na sisi tumeshika makali, tukitikisika tutajiumiza wenyewe," anafanunua Bi Nduna.

Hivyo basi, anasema, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu, wananchi wa Jimbo la Kilombero wakafanye uamuzi wa busara kwa kuwachagua wagombea wa CHADEMA wa ngazi za udiwani, ubunge na urais.

"Wakati umewadia kwa wananchi kutumia vema shahada za kupiga kura na kufanya maamuzi yenye busara, kuchagua viongozi bora, ambao hawatokani na chama kile kile, chenye uozo ulele," anasema Bi Nduna.

Anasema, CHADEMA itailetea nchi mabadiliko ya kweli, uhuru wa kweli na kiongozi bora atatoka katika chama hicho na kwamba mifano hai inaonekana katika halmashauri inazoziongoza za Hai, Karatu na Kigoma Ujiji.

Kwa jimbo la Kilombero, Bi Nduna anasema anahitajika mbunge atakayesimamia vizuri sekta za kilimo, afya, elimu, soko, mikopo, barabara na ajira.

Hivyo basi, ahadi zake kwa wana wa Kilombero ni pamoja na kuwajibika kuhakikisha kuna ongezeko la ajira kwa kusikiliza mawazo ya makundi mbalimbali na kujadili kwa pamoja ili kupata ufumbuzi.

Katika kushughulikia tatizo hilo, anasema ni muhimu vipaji vya vijana vikaendelezwa, ili wawe wabunifu na waweze kuanzisha miradi na kujiajiri.

Pia anasema zinahitajika zana za kisasa ili kuleta mapinduzi ya kweli katika kilimo ambacho kwa sasa kinatumia jembe la mkono hivyo kuwa cha suluba na kuwafanya vijana wengi kukimbilia mijini.

Wawekezaji watakaribishwa katika Jimbo la Kilombero lakini, ni lazima washirikiane na wenyeji ambao wengi ni wakulima na si kuwanyanyasa, anasema mgombea huyo.

Anasema wataalamu wa kilimo nchini watatumiwa ili kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima kwa ajili ya kuzalisha kwa wingi mazao bora.

Mgombea huyo anaahidi kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao kwa kushirikiana na vyama vya ushirika, wafanyabiashara wa ndani na nje, ili wapate bei nzuri.

"Nitahimiza uwajibikaji na usimamizi mzuri wa mafungu yanayotengwa kwa afya, yaani ujenzi wa vituo vya afya na kuhakikisha madaktari, wauguzi, dawa na vifaa vinakuwepo kwenye vituo vya afya," anasema.

Kipaumbele kingine anachokitaja Bi Nduna ni kuhakikisha elimu ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake inatolewa. Anasema pia atahamasisha na kusimamia kuwepo kwa madarasa ya kutosha, walimu, vitabu na wakaguzi wa elimu wanaowajibika.

Pamoja na kusimamia ongezeko la shule za msingi vijijini, Bi Nduna anasema ni muhimu katika zama hizi za sayansi na teknolojia kila kata ikawa na shule ya sekondari hadi kidato cha nne na kila tarafa ikiwa na sekondari hadi kidato cha sita.

Je, atawezeje kufanikisha ahadi zake hizo? Bi Nduna anasema; nguvu za wananchi watakaokuwa wamehamasika kujiletea maendeleo ni jambo la msingi katika kufanikisha ahadi hizo.

Fedha zitakazokuwa zinakusanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, atahakikisha anazisimamia vyema ili zitumike kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na jimbo la Kilombero.

"Naahidi kutoa asilimia tano ya mshahara wangu kila mwezi, kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya jimbo langu," anajitolea Bi Nduna.

Kumekuwepo na baadhi ya watu ambao hukopa fedha kwa ajili ya kuendesha miradi lakini wengine wamefikia mahali wamefilisiwa kwa kushindwa kuirejesha, Bi Nduna anasema chini ya uwakilishi wake, iwapo atakuwa mbunge, atahakikisha kunatolewa elimu ya kutosha ya jinsi ya utumiaji wa mikopo na kusimamia upatikanaji wake.

Ujenzi wa barabara kuu na za vijiji ni kipaumbele chake, kwani kwa kuwepo miundombinu hiyo wananchi wataweza kujiletea maendeleo kwa haraka.

"Nataka kuonesha na kuthibitisha kwamba, wanawake tukipata nafasi na ushirikiano, tunaweza kuongoza," anasema kwa uhakika.

Hata hivyo, Bi Nduna anasema kina cha maji hayo ambayo ameshayavulia nguo ni kirefu hususani kwa wagombea wa vyama vya upinzani ambavyo havina pesa.

Anasema ubunge kupitia jimboni unahitaji fedha nyingi kwa ajili ya mambo mengi kama vile usafiri na vifaa vya kampeni mathalani vipaza sauti, mabango, vipeperushi na fulana.

Bi Nduna ambaye alizaliwa Desemba 29, 1961, amepata mafunzo ya uhasibu na uchapaji baada ya kumaliza elimu ya sekondari, na kwa sasa ni katibu wa kikundi cha Tulingane na Ofisa Kurugenzi ya Wanawake CHADEMA. Anaamini mbunge ajaye wa Kilombero ni yeye.