Na Tausi Ally
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa, leo anaanza ziara ya kikazi ya siku tano katika Mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Nduli, Waziri Mkuu atakwenda Ikulu ndogo kupokea taarifa ya mkoa na kisha ataelekea Kitonga, Wilaya ya Kilolo kukagua mradi wa umwagiliaji maji.Taarifa hiyo ilisema kuwa baadaye atakwenda Ruaha Mbuyuni ambako ataweka jiwe la msingi katika soko la vitunguu na mchana atahutubia mkutano wa hadhara na kisha atakwenda kukagua daraja la Msosa lililoko Ruaha Mbuyuni.
Septemba 26, atakuwa wilayani Iringa ambako amepangiwa kufungua banio la mfereji la Mlenge na kusalimiana na wananchi na kisha kuelekea Pawaga kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari Pawaga, kabla ya kwenda Kitanzini kukagua shughuli za Saccos ya vijana.Jioni atahubia wananchi katika Uwanja wa Samora Iringa mjini na usiku atafanya mazungumzo na wawakilishi vijana na siku ya Jumatano ataweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari Changarawe iliyoko Mafinga, wilayani Mufindi.
Baada ya hapo atakwenda Mtambula ambako atazindua ghala na kukabidhi hundi kwa wana Saccos na anatarajiwa kutembelea vitalu vya chai vya wakulima wadogo wadogo wa Lufana.Jioni siku hiyo, atahutubia wananchi katika uwanja wa Mashujaa Mafinga na usiku amepangiwa kukutana na wafanyabiashara na wawakilishi wa wenye viwanda.
Siku ya Alhamisi asubuhi ataelekea Matamba, wilayani Makete ambako atapokea maelezo ya mradi wa umeme ulioko Madinahi na mchana atakwenda Bulongwa kutembelea kituo cha watoto yatima na jioni atahutubia wananchi Bulongwa.
Siku ya Ijumaa Lowassa atakuwa Njombe ambako ataweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi Mabatini, kukagua kiwanda cha maziwa na kisha atakwenda kukagua Saccos ya Mtwango. Akitoka huko atakwenda Makambako kukagua ujenzi wa kituo cha umeme, na baadaye atakwenda TFC kukagua maghala ya mbolea kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Polisi.
Jioni atarudi Iringa mjini ambako usiku amepangiwa kukutana na akinamama wajasiriamali. Anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam Jumamosi asubuhi.