Na Muhibu Said
WAKATI Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema akiwa katika juhudi za kulisafisha jeshi hilo, baadhi ya askari wa Kituo cha Oysterbay, wanadaiwa kula njama za kutaka kumfutia kesi kinyemela mkazi mmoja wa Kinondoni Moscow anayetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Hananasif, jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka kituoni hapo zinaeleza kuwa, askari hao wanakula njama hizo kwa kushirikiana na baadhi ya watu wa karibu na mtuhumiwa ambaye ni baba mlezi wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa).
Wasiwasi wa kufutwa kwa kesi hiyo kinyemela na kinyume cha sheria ya mwaka 1998 ya makosa ya kujamiiana, unakuja baada ya mtuhumiwa, jina tunalo kuachiwa huru na askari wa kituo hicho katika mazingira ya kutatanisha.
Mbali na kuachiwa huru, mtuhumiwa pia anadaiwa kushauriwa kuhama katika nyumba aliyokuwa akiishi awali, kufanya mipango ya kumhamisha mtoto shule na kumjengea mlalamikaji wa kesi hiyo mazingira ya kupoteza ushahidi.
Inadaiwa kuwa baada ya kupewa ushauri huo, mtuhumiwa na mkewe ambaye ni shangazi wa mtoto huyo, wametelekeza vyombo vyao vya nyumbani katika chumba walichokuwa wakiishi na kuamua kuishi kwa kujificha. Wazazi wa mtoto huyo wanaishi mkoani Morogoro.
Kutokana na kushauriwa hivyo, inadaiwa kuwa hivi sasa mtuhumiwa na mkewe, wanaishi mafichoni maeneo ya Tegeta, jijini Dar es Salaam.Mtuhumiwa alikamatwa Septemba 2, mwaka huu na kushikiliwa siku hiyo katika kituo kidogo cha polisi cha Kinondoni Hananasif ambako jalada Na. KH/RB/1045/2006 lilifunguliwa na hati ya polisi ya kupata matibabu (PF3) ilitolewa kwa mtoto huyo ambaye alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kupimwa.
Taarifa za tukio hilo ziliwasilishwa kituoni hapo na baba mdogo wa mtoto huyo, Dismas Elias ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo.Baadaye, Septemba 3, mtuhumiwa alipelekwa katika kituo cha polisi Oysterbay ambako jalada Na. OB/RB/15191/2006 lilifunguliwa.Hata hivyo, siku iliyofuatia aliachiwa huru licha ya ripoti ya daktari kutoka hospitali hiyo kuonyesha kuwapo kwa tukio la kubakwa kwa mtoto huyo.
Mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Ijumaa Septemba mosi, mwaka huu, usiku, ambapo mtoto alipaza sauti ya kilio kutokana na maumivu aliyoyapata.Baada ya kitendo hicho, inadaiwa mtuhumiwa aliamka asubuhi mapema na kuondoka, akimwamcha mtoto nyumbani wakati huo mkewe alikuwa safarini.
"Majirani walilazimika kumhoji mtoto kulipopambazuka, ndipo mtoto aliyebakwa akaeleza kuwa baba yake alikuwa akimbaka. Kesi hiyo iliripotiwa polisi ndipo polisi walikuja na kumkamata mtuhumiwa. Hata hivyo, siku ya Jumatatu jioni mtuhumiwa alirudi kutoka polisi katika mazingira yanayoonyesha rushwa imetumika," kilieleza chanzo chetu cha habari.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jamal Rwambow, alipoulizwa, awali, hakukiri walakukanusha taarifa hizo, badala yake aliomba apewe muda ili apate kulifuatilia suala hilo kwa kina.
"Inawezekana wakubwa hawajui kabisa suala hilo. Ngoja nitamuuliza OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) na OCS (Mkuu wa Kituo), kisha unitafute baadaye," alisema Kamanda Rwambow.Baadaye, Kamanda Rwambow, aliwasiliana na Mwananchi kwa njia ya simu na kusema kuwa amechunguza jalada la kesi hiyo na taarifa za awali zinaonyesha kuwa upo mchezo unaoonekana kufanywa katika kesi hiyo.
"Nimepata jalada, nimeingiwa na wasiwasi na mchezo unaochezwa katika staili ambayo haijulikani anayehusika kati ya askari wangu ama nani," alisema Kamanda Rwambow.Kamanda Rwambow, alisema kwa mfano, maelezo yaliyomo katika jalada hilo, yanaonyesha mtoto anayedaiwa kubakwa akikanusha kufanyiwa kitendo hicho, huku mtu aliyetoa taarifa za tuhuma hizo polisi Sepetmba mosi, akizikanusha baadaye Septemba 4, mwaka huu.
Alisema kwingine kunakoonekana kuchezewa, ni katika hati ya polisi ya matibabu (PF3) na katika ripoti ya vipimo alivyofanyiwa mtoto huyo katika Hospitali ya Mwananyamala.Kamanda Rwambow, alisema wakati nakala ya PF3 ambayo Mwananchi inayo inaonyesha kujazwa katika kituo kidogo cha polisi Kinondoni Hananasif, nakala iliyopo katika jalada hilo la polisi, inaonyesha kwamba, haikujazwa.
Alisema pia nakala za ripoti ya vipimo ambayo Mwananchi inayo, inaonyesha kwamba, mtoto huyo alibakwa, lakini ile iliyoko polisi inaonyesha kuwa hakukutwa na mbegu wala michubuko, ingawa hakuwa na bikira.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Rwambow, alisema amewaagiza wataalamu wake kuendelea na uchunguzi ili kupata ukweli juu ya suala hilo.