Na Mwandishi Wetu
WAKATI kukiwa na taarifa kwamba serikali ina mpango wa kuzirejesha nyumba zake zilizouzwa kwa baadhi ya watumishi wa umma katika serikali iliyopita, Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, John Kijazi, amesema wizara hiyo haijapata maelekezo kutoka mamlaka za juu yakiagiza utekelezaji wa uamuzi huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kijazi alisema kama wizara itapata maelekezo hayo, basi itayafanyia kazi."Wizara ya Miundombinu haijapata maelekezo kutoka mamlaka za juu yanayotaka nyumba za serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma zirejeshwe," alifafanua Kijazi.Kijazi alisema hatua iliyopo ni kwamba wizara imetoa siku 30 kwa Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kuhakikisha watumishi wote wa umma waliokopeshwa nyumba wanalipa fedha zilizobaki."Tumeamua watumishi wote ambao walikopeshwa nyumba walipe madeni yao," alisema Kijazi.
Kwa mujibu wa agizo hilo kwa TBA lililotolewa Ijumaa wiki iliyopita, linawataka watumishi wote wa umma waliokopeshwa nyumba hizo kulipa madeni yao kama mikataba inavyojieleza.Agizo hilo linafanua zaidi kwamba, mtumishi atakayeshindwa kulipa deni hilo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutenguliwa kwa mkataba wa ununuzi.
Kumekuwa na minong'ono kuwa serikali ya awamu ya nne inapanga kuwanyang'anya baadhi ya watu waliouziwa nyumba za serikali ambazo sasa zimesababisha uhaba wa nyumba kwa watumishi wa serikali nchi nzima.Minong'ono hiyo imeendelea kushika kasi hata baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwahakikishia watu walionunua nyumba hizo kuwa hawatanyang'anywa akisema hata yeye ni miongoni mwa watu walionunua chini ya mpango huo.
Hata hivyo, serikali ya awamu ya nne imesema nyumba zilizojengwa katika siku za karibuni na ambazo sasa zinatumika kama makazi y watumishi wa umma, wakiwamo mawaziri, hazitauzwa tena.Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ilianzisha utaratibu wa kuwauzia nyumba za serikali baadhi ya watumishi wake, hatua ambayo ilizusha mjadala mkubwa miongoni mwa Watanzania.
Baadhi ya watu waliita hatua hiyo ni ya kuwapa bure nyumba watumishi hao kutokana na kuuzwa kwa bei ya kutupwa.Akiwa Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, ambaye sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mara kwa mara alitetea sera hiyo ya serikali ya awamu ya tatu akielezea kwamba ililenga kuwapa makazi bora watumishi wa umma