Na Mussa Juma, Arusha HIFADHI ya Taifa ya Arusha (ANAPA), imekitaka Chama cha Wapagazi wa Mlima Meru kuwaelimisha wanachama wake kutoa huduma bora kwa wageni wanaopanda mlima huo, vinginevyo watazuiwa kutoa huduma hiyo.
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Erastus Lufungilo alitoa wito huo juzi wakati akizungumzia malalamiko ya wamiliki wa kampuni za utalii kuwa baadhi ya wapagazi wamekuwa wakitoa huduma mbaya kwa watalii na hivyo wanalazimika kuja na wapagazi kutoka mjini Arusha au Moshi.
Alisema kutokana na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu wapagazi, hifadhi hiyo inakusudia kutoa mapendekezo kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuruhusu wapagaji wengi ambao hawatoki katika chama hicho kutoa huduma.
"Mwelekeo wetu wa baadaye ni kufanya shughuli za upagazi kuwa sawa kama ilivyo katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro,lakini makampuni ya utalii yakianza kuleta wapagazi tuna imani idadi kubwa itatoka kwa wapagazi wanaoishi jirani na mlima huu,"alisema.
Alisema ANAPA itaendelea kukisaidia chama cha wapagazi wa Mlima Meru katika kutoa elimu kwa wanachama wake ili waboreshe huduma zao kwa wageni na hatimaye kuingia katika ushindani.
Naye, Mwenyekiti wa chama hicho cha wapagazi hao wa Mlima Meru,Tutason Ako akizungumzia malalamiko hayo, alisema ni kweli yamekuwa yakitolewa, lakini wao kama viongozi pia wamekuwa wakitoa elimu kwa wanachama wao.
"Sisi kama chama tunajitahidi, wanachama wetu watoe huduma bora, lakini kama kuna matatizo ni madogo madogo ambayo tunaimani yatakwisha,"alisema Ako.
Mawakala wa watalii na wamiliki wa makampuni ya utalii wamekuwa kwa muda mrefu wakilalamikia wapagazi wa kutoka eneo linalozunguka mlima huo kuwa wamekuwa wakifanyakazi chini ya kiwango na hivyo kuathiri utalii wa kupanda mlima huo.