Na Boniface Meena
WATUMISHI watatu wa ubalozi wa Burundi jijini Dar es Salaam wamedai ubalozi huo umewafukuza kazi kinyume cha sheria.Wafanyakazi hao, Joseph Tomola, Mathias Lukoma ambao ni walinzi wa ubalozi huo na Siita Sanga ambaye ni mfagizi ndani ya ubalozi huo walidai kutimuliwa kazi Ijumaa wiki iliyopita.
Wafanyakazi hao wanadai walifukuzwa kazi ijumaa bila kupewa barua rasmi pamoja na mshahara wa mwezi mmoja na fedha za kuhamisha mizigo yao.Walinzi hao wawili walidai kuwa wamefukuzwa kazi na balozi wa Burundi, Amuri Bugengwanubusa kwa madai kuwa walishindwa kulinda vizuri ubalozi na kusababisha mhalifu kuingia na kusababisha hitilafu ya umeme ubalozini hapo ambayo ingeweza kuunguza majengo ya ubalozi huo pamoja naye (balozi).
Kwa upande wa Sanga, yeye alidai kufukuwa kazi kwa madai ya kutoonekana kazini , ingawa alidai kuwa alikuwa mgonjwa. Alidai kuwa aliwasilisha barua ya kuelezea ugonjwa wake, lakini balozi huyo hakumsikiliza.Wakizungumza na Mwananchi Jumapili, watumishi hao walisema baada ya tukio hilo la hitilafu walimtaka balozi huyo kuwashtaki polisi kama kweli wamekosea, lakini alikataa.
“Tulitaka tufikishwe polisi ili waweze kuchunguza na kuupata ukweli, lakini yeye alikataa, sisi hatukusababisha hitilafu yoyote na tulilinda ubalozi kama kawaida,” alisema TomolaAkizungumza na Mwananchi Jumapili ofisini kwake kuhusu kufukuzwa kwa wafanyakazi hao, Balozi Amuri alisema amefikia uamuzi huo ili kulinda mali za ubalozi wake zinazotumiwa vibaya na wafanyakazi hao.
Alisema Septemba 14, walinzi hao hawakufanya kazi ya ulinzi wa ubalozi huo ipasavyo kwa kushindwa kumbaini mhalifu aliyeingia na kukata na kuharibu nyaya za umeme akitumia mshumaa na kusababisha hitilafu ya umeme.Alisema walinzi hao walishindwa kumwona mhalifu huyo na kuongeza kuwa uharibifu uliofanywa na mhalifu huyo ulisababisha ubalozi kutofanya kazi Septemba 15 kwa kutokana na kukosa umeme.
Alisema kuwa hakutaka kuwapeleka polisi kwani kufanya hivyo ingekuwa ni usumbufu kwa polisi kufuatilia kitu kama hicho ambacho alikuwa anao uwezo wa kuchukua hatua yeye mwenyewe.“Mimi nimekuja hapa nina miezi miwili sasa, Ijumaa nilikuja hapa nikakuta nyaya kwenye main switch zimekatwa na jenereta haifanyi kazi nilipowauliza walinzi hapa wakaniambia wao hawajui chochote, kutokana na jibu hilo nikaamua kuwafukuza siku hiyo”,alisema Amuri.
Kuhusu kumfukuza mfagizi, balozi huyo alisema: “Mimi ninafanya kazi kwa kufuata utaratibu, nimekuja hapa kuchukua nafasi ya balozi aliyeondoka (Mbonayo Alois), kuwafukuza hawa ni kutokana na matatizo yao, barua niliwapa siku niliyowafukuza,”alisema Amuri.Hata hivyo, habari kutoka ndani ya ubalozi huo, zinaeleza kuwa baada ya mwandishi wa gazeti hili kwenda kufuatilia habari hiyo, juzi mchana, balozi huyo aliandaa barua kwa ajili ya kuwapatia wafanyakazi hao bila mafao yao.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili juzi jioni, balozi mdogo wa Burundi, Juvenile Hatungimana alisema: “Sasa hivi Amuri ameniletea barua za kuwafukuza kazi ili niwape baada ya wewe(Mwandishi) kufuatilia suala hili”.Barua hiyo ambayo Mwananchi Jumapili inayo nakala yake inaonyesha wafanyakazi hao wamefukuzwa kazi Ijumaa, ingawa hadi jana jioni wafanyakazi hao walikuwa hawajakabidhiwa barua hiyo.