Na Ally Sonda,Moshi
WAZIRI wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu juzi alikuwa miongoni mwa watazamaji walioshuhudia maonyesho ya kupambana na vitendo vya ugaidi yaliyofanywa na askari polisi waliokuwa kwenye mafunzo maalumu ya kupambana na ugaidi.
Maonyesho hayo yalikuwa ni sehemu ya ufungaji wa maafunzo hayo ya wiki sita yaliyojumuisha askari polisi wanaume 22 na mwanamke mmoja kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Katika maonyesho hayo yaliyofanyika kwenye eneo la kulenga shabaha la Chuo cha Polis (CCP) kwenye kijiji cha Mabogini,wilayani Moshi vijijini,Waziri Mwapachu aliona jinsi ya kuokoa watu waliotekwa na magaidi, kulenga shabaha na jinsi ya kupambana na magaidi ana kwa ana.
Akifunga mafunzo hayo, Mwapachu aliishukuru Marekani kwa msaada mkubwa inaoutoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali za kupambana na uhalifu hususan wa vitendo vya ugaidi ambavyo hivi sasa vinatishia dunia.
Aliwataka askari waliopata mafunzo hayo yaaliyofadhiliwa na Marekani kuwa dira ya kuongoza vita dhidi ya ugaidi nchini ili kujijengea heshima kwa wafadhili waliojitolea kufanikisha mafunzo hayo muhimu.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Michael Ratzer alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania kuimarisha ulinzi wa raia wake kadri itakavyoweza na hususan katika vita vya kupambana na tishio la ugaidi.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na wakufunzi wa Kimarekani. Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa mbalimbali wa polisi kutoka makao makuu na Mkuu wa CCP,Josia Mwesiga.