Na Waandishi Wetu
DALILI za kuwepo kwa kiasi kikubwa cha akiba ya mafuta katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Tanzania zimezidi kupata nguvu na kudhihirika na kuvutia kampuni nyingi za kimataifa kufika kwa ajili ya kutafiti nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi.
Hilo, linaelekea kuleta matumaini mapya katikaTanzania ambayo inakabiliana na hali mbaya ya ukosefu wa nishati, hasa umeme na kushuhudia ongezeko kubwa la bei ya mafuta na bidhaa za petroli, ambalo limeziathiri pia sekta nyingine.
Mkataba wa hivi karibuni kabisa ambao umeingiwa na serikali ni ule baina yake na kampuni ya Petrodel Resources ya Uingereza iliyoingia mkataba wa miaka 11 ili kutafiti mafuta mkoani Tanga na maeneo ya Kimbiji na Latham, wilayani Temeke.Chini ya mkataba huo, endapo kampuni hiyo itamaliza kazi yake na kupata mafuta, itaanza uzalishaji wa nishati kwa kipindi cha miaka 25 na baadaye kuongezewa miaka 20 na kufanya jumla ya kipindi cha uzalishaji kuwa miaka 45.
Mikataba hiyo miwili, mmoja ukiwa wa kutafiti mafuta Tanga na mwingine Dar es Salaam, ilisainiwa jana jijini kati ya Waziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha na Rais wa Petrodel Resource, Dk Philip Nelson, huku kila upande ukiwa na mashahidi.Mkataba mwingine ulioingiwa ni ule wa utafiti wa mafuta katika bonde la Ruvuma, kusini mashariki mwa Tanzania.
Katika mkataba huo serikali iliingia mkataba wa utafiti na kampuni ya utafiti na uchimbaji ya kampuni tanzu ya Ndovu Resources Limited (“Ndovu”) ambayo ni kampuni tanzu ya Aminex PLC ya London, ambapo taarifa zingine zinaeleza kuwa kampuni hiyo, imetangaza kusaini mkataba na kampuni nyingine ya uchimbaji mafuta na gesi ya Hardman Resources Ltd. (“Hardman”), ya Australia .
Akilizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Utafiti, Uzalishaji na huduma za kiufundi wa Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), alfani Halfani, alisema Kampuni ya Aminex imeingia ubia na Hardman ya Australia yenye miradi kama hiyo nchini Uganda.
lisema sheria inaruhusu kampuni kufanya hivyo baada ya kumuomba kibali waziri mhusika na kwamba TPDC Inaelewa juu ya ubia huo.Alisema kampuni ya Aminex wameshafanya nao kazi hapa nchini na wana uwezo wa kazi hiyo na kuwa suala la kuingia ubia ni kwa ajili ya kujizatiti na au kupata nguvu zaidi ya kufanikisha kazi yao.Alisema kazi katika bonde hilo inafanyika vizuri na kuwa mwezi uliopita wataalam wa jiolojia kutoka katika shirika hilo na wale wa kampuni hiyo walikwenda kwenye eneo kuliona lilivyo hali inayoamaanisha kuwa kazi imeanza.
Mkataba huo, utaiwezesha kampuni ya Hardman kujipatia kiasi cha riba ya asilimia 50 katika mkataba wa ushirikiano wa uzalishaji wa Ruvuma (“PSA”) kwa makubaliano ya ulipiaji wa gharama wa asilimia 100 wa gharama za utafiti wa mafuta unaokadiriwa kufikia kiasi cha dola za Kimarekani 3,000,000.
Baada ya kumalizika utafiti huo makubaliano yanatarajiwa kuwa umiliki wa hisa asilimia 50 kwa 50 kwa kampuni za Ndovu na Hardman.Utafiti huo wa mafuta unatarajiwa kufanyika katika eneo la zaidi ya kilomita 500 na unatarajiwa kufanyika mwaka huu kwa kuanza kuchimba visima katika eneo hilo.
Eneo hilo la utafiti lipo kilomita 500, kusini mwa Dar es Salaam kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji na linatawanyika hadi Mtwara na Lindi, likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 12,360, linafahamika kama bonde la Ruvuma kwa upande wa Tanzania.
Eneo hilo lipo karibu kabisa na eneo ilipo Mnazi Bay linaloendelezwa hivi sasa tangu wakati huo hadi sasa yameshapatikana mafanikio katika utafiti wa gesi. Lengo kubwa ni kutafiti mafuta yaliyopo katika eneo hilo yanayotarajiwa kuwa katika kina cha mita kati ya 1,000 na 3,000. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Yona Killagane, mpaka sasa kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta na shughuli zinazorendana na hizo zimefikia 13.
Alisema serikali inaendelea kutoa leseni kwa ajili ya utafiti wa maeneo watakayohisi kuwa na mafuta. Akizungumzia Pemba na Zanzibar, Killagane alisema kampuni ya Antrim Resource imeshateuliwa lakini haijapewa leseni.Kampuni za kigeni ambazo zimeshasaini mikataba na serikali ya Tanzania, miongoni mwao zipo kampuni ya utafiti mafuta ya Petrobras ya Brazil, inayofanya utafiti kwenye kitalu namba 5, mashariki mwa Mafia; Orphir Energy ya Australia inayofanya utafiti katika kitalu 1, mashariki mwa Mtwara; Ndovu Resources (Australia)kwenye bonde la Ruvuma na Nyuni mashariki.
Nyingine ni Songosongo; na Artumas Group za Canada zenye leseni ya kuendeleza uchimbaji gesi katik eneo la Mnazi Bay.Pia zipo kampuni za Maurel na Prom za Ufaransa, zinazofanya utafiti huko Bigwa na kwenye mkondo wa Mafia channel, Antrim Resources ya Canada, inayofanya utafiti visiwani Pemba na Zanzibar , na PanAfrican Energy inayoshirikiana na Songo Songo.Na Mkataba wa hivi karibuni kabisa kusainiwa ni ule uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni la Dominion Oil and Gas itakayofanya utafiti huko Kisangire, mkoani Pwani, Madawa mkoani Lindi na katika eneo la mbuga za Selous.