Na Lilian Lugakingira, Bukoba
MTOTO Blavias Godpride (14), mkazi wa Kyasha, Kata ya Buhembe katika Manispaa ya Bukoba, amefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi wakati akichimba mchanga wa kuuza ili apate fedha za kufanyia sherehe.
Mtoto huyo ambaye amemaliza darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Nyakato, iliyoko katika manispaa hiyo, alikwenda kuchimba mchanga katika eneo la Kashekulo kwa ajili ya kuuza.
Imedaiwa kuwa kutokana na uwezo mdogo wa wazazi wake, alishindwa kupata fedha za kujumuika na wenzake kujipongeza baada ya kumaliza mtihani wa taifa wa darasa la saba, uliomalizika Septemba 14, mwaka huu, aliamua kuanza shughuli za kuchimba mchanga wa kuuza ili apate fedha za sherehe hiyo.
Wakati mtoto huyo akichimba mchanga pamoja na wenzake, udongo uliporomoka na kumfukia na shughuli za kumwokoa zilifanyika, lakini alipotolewa katika kifusi hicho, alikuwa amekwisha fariki.
Mwili wa mtoto huyo ulichukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Adihaki Rashid, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.