Na Mussa Haji Foum, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar ataajiri walimu wapatao 3,000 wenye shahada na stashahada, kwa ajili ya shule za sekondari, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, alisema katika kipindi hicho, walimu 1,200 wenye shahada na1,500 wenye stashahada, wataajiriwa ili kuondoa tatizo la walimu visiwani humo na hasa walimu wa masomo ya sayansi.
Alisema serikali inaendelea na jitihada zake za kuwaelimisha wananfunzi katika vyuo vikuu viliopo Zanzibar, ikiwa pamoja Chuo Kikuu cha Ualimu cha Chukwani na Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu.
Waziri Haroun alisema katika kipindi hicho, serikali inakusudia kujenga shule kumi za secondari za kisasa, zitakazoanzia na kidato cha kwanza hadi cha sita.
Alisema shule hizo zitakuwa na maabara za kisasa, vyumba vya komputa, viwanja vya michezo kwa wanafunzi wanawake na wanaume.
Aliongeza kuwa hatu hiyo, itawawezesha wanafunzi watakaofaulu kuingia kidatu cha tano kujiunga na shule hizo na kuondokana na usumbufu wa kufuata masomo mijini.
Alifahamisha kuwa vyuo vya elimu mbadala, vitajengwa katika maeneo ya Mkokotoni Unguja na Vitongoji kisiwani Pemba, ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliokosa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbali mbali.