Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waziri Mkuu Lowassa atetea safari za Rais Kikwete
Waziri Mkuu Lowassa atetea safari za Rais Kikwete
By Habari Tanzania | Published  09/22/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Irene Bwire, Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU, Edward Lowassa amezitetea safari za nje ya nchi anazofanya Rais Jakaya Kikwete kuwa zimelenga kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania haraka na kupunguza matatizo yanayowakabili Watanzania.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Mto wa Mbu katika mkutano wa hadhara kuwa kitendo cha kumwambia Rais asiende nje ya nchi na badala yake abaki kushughulikia matatizo ya umeme ni sawa na kumdhihaki.

"Katika magazeti ya leo, kuna kiongozi wa CUF amekaririwa akimweleza Rais aje nchini ashughulikie matatizo ya umeme, kwa kweli huko ni kumdhihaki…", alisema Waziri Mkuu.

"Tunakubali kwamba tatizo la umeme lipo lakini hatukulisababisha sisi… ni tatizo lilitokana na kuwa na chanzo kimoja tu cha umeme.. juzi nimesema tunatambua adha wanayoipata wananchi na tayari tumeagiza mashine za kutosheleza umeme katika miezi michache ijayo," alisema.

"Nataka niuhakikishie umma kuwa ifikapo Jumanne megawati 35 zilizopotea zitakuwa zimerudi, pia kuna jitihada za kuzalisha megawati 12 na nyingine nane katika muda si mrefu…," alisisitiza

Kuhusu safari za Rais za nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema ziko za aina tatu na kwamba ya kwanza ni ile ya kujitambulisha kwa majirani zake na nchi ambazo zamani zilikuwa wanachama wa nchi zilizo mstari wa mbele na sasa hivi ni za SADC.

Alisema aina nyingine ya safari ambazo Rais amefanya ni kuhudhuria mikutano ya viongozi wenzake ambao ni wakuu wa nchi na aina ya tatu ni ziara za kutafuta misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. "Safari kama hizi alizifanya Uarabuni, Ulaya na Marekani."

Alisema anachofanya Rais Kikwete hivi sasa ni mawindo ya kiuchumi na diplomasia ya kiuchumi na kutoa mfano kwamba msitu wenye swala na sungura wengi hivi sasa uko Marekani hivyo ni lazima aende huko.

Alisema kutokana na ziara za mwanzo alizofanya Rais huko Uarabuni na Marekani, Tanzania imeweza kupata ufadhili wa kujenga Chuo Kikuu kingine Dodoma na ahadi ya ujenzi wa barabara ya kutoka Kigoma hadi Manyoni kwa kiwango cha lami. "Asingeenda huko vingetoka wapi?, alihoji Waziri Mkuu.

Kuhusu ziara ya sasa, Waziri Mkuu alisema Rais Kikwete ndiye Rais pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambaye alipata muda wa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani, George W. Bush. Pia Rais Kikwete alipewa nafasi ya kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa hapo jana ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ashike madaraka.

Alisema Marekani imeanzisha Akaunti ya Milenia (Millenium Challenge Account) ambayo inachangiwa fedha na serikali ya nchi hiyo ikiwa ni mpango wa kusaidia nchi zinazoendelea ambazo zinatimiza masharti ya utawala bora na vita dhidi ya rushwa. Chini ya akaunti hii, Tanzania imeomba karibu sh. bilioni moja (dola za kimarekani milioni 798).

Alisema katika mazungumzo yake na Rais Bush, Rais Kikwete ametumia fursa hiyo kumwomba aharakishe upatikanaji wa fedha hizo kwani serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kutoka Mugumu hadi Mto wa Mbu kupitia Loliondo kwa kutumia kiasi cha fedha hizo. Alisema nia ya barabara hiyo ni kuepusha msongamano wa magari katika hifadhi za taifa za Serengeti na Ngorongoro.

Alisisitiza kuwa Rais anapondoka nchini haimaansihi kuwa kazi nyingine zimelala, bali zinaendelea kama kawaida. "Ieleweke kuwa Rais akiondoka shughli za Serikari hazisimami, Makamu wa Rais yupo, Rais wa Zanzibar yupo na mimi pia nimo nimo, na akiwa na jambo la haraka, Rais haachi kupiga simu au kutuma sms na mambo yanakwenda…"

Alisema anachofanya Rais Kikwete katika ziara hizo si kupoteza muda bali alimtaka mtu anayemwambia Rais asifanye ziara hizo, akae pembeni, ajipumzishe na aiachie CCM ifanye kazi ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba amesema anamshukuru Mungu kwa vile yeye na Waziri Mkuu wanamsaidia kazi mtu mmoja, yaani Rais Jakaya Kikwete. "Wewe uko serikalini na mimi niko katika chama."

Alisema umri wake si kigezo cha kumzuia kufanya kazi na ameahidi kutumia nguvu na uwezo wake wote kuhakikisha kazi yake inafanyikaa. "wenzangu wa umri wanaambiwa wakapumzike mimi napewa kazi mpya… na kama kazi inaua, basi mwaka huu iniue," alisema.

Alisema alipoteuliwa, alielezwa na mwenyekiti kwamba aende makao makuu kupaboresha na asialike wazee wenzake.

"Kwa hiyo najua ninapaswa niandae vijana wa kuchapa kazi, niwafundishe kazi na kuwaanda kushika nafasi nitakapopumzika…" alisema.

Alisema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kumfundisha kazi tangu akiwa Katibu Mtendaji wa CCM wilaya ya Monduli na wakati huo Waziri Mkuu alikuwa Katibu Mtendaji wa CCM wa Mkoa wa Arusha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.