Na Mpoki Bukuku
MAKALI ya mgawo wa umeme yanatarajiwa kuanza kupungua leo baada ya kampuni ya Songas kufunga injini ya kukodi katika mtambo wake wa megawati 40 ulioharibika mwezi uliopita.
Kuharibika kwa mtambo huo kulisababisha kupungua kwa umeme katika gridi ya taifa na kuongeza makali ya mgawo kutoka siku tatu hadi tano kwa wiki.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Songas, Phil Masson, alisema injini hiyo ambayo imekodiwa nchini Uholanzi iliunganishwa jana na inaanza kutumika leo kwa majaribio ili Jumatatu iwe inafanya kazi kamili ya kuzalisha megawati 40.
Mafundi wa Kampuni ya General Electronics (GE), wamewasili nchini na kutwa nzima jana walikuwa wakihangaika kuifunga injini hiyo katika mtambo huo, kabla ya kuanza kuijaribu leo.
Alisema injini nyingine ya megawati 35 ambayo iliharibika wiki iliyopita na kuongeza mgawo, imetengenezwa na pia inaanza kufungwa leo. Matarajio ni kwamba kesho itajaribiwa kabla ya kuanza kuzalisha umeme Jumatatu.
Kwa maana hiyo hadi Jumatatu megawati 75 za umeme zitakuwa zimeingizwa katika gridi ya taifa na kupunguza makali hayo.
"Tumechukua hatua za dharura kuagiza injini hii ya kukodi ili kupunguza makali ya mgawo, kwa hiyo tuna uhakika ifikapo mwanzoni mwa wiki ijayo tutakuwa tumaliza kazi rasmi, " alisema.
Alisema injini iliyokwenda Uholanzi kufanyiwa matengenezo itarudishwa katikati ya mwezi ujao na hivyo kufanya mtambo huo kufanya kazi kwa uwezo wake wote muda huo.
Endapo maelezo hayo tayafanikiwa kama yalivyopangwa, mitambo hiyo itakuwa imetengamaa kabla ya muda uliokuwa umepangwa.
Wakati injini ya megawati 40 ilitarajiwa baada ya mwezi mmoja zaidi, ile ya megawati 35 ilitarajiwa kukamilika kwa wiki moja zaidi.