Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Saddam, Bush mahasimu wanaoshabihiana.
http://www.habaritanzania.com/articles/1060/1/Saddam,-Bush--mahasimu-wanaoshabihiana.
By Nthelezi Nesaa
Published on 09/22/2006
 
Katika kutafakari mambo na hali inavyoendelea nchini Irak,safu hii imeonelea ijaribu kutoa mpambano wa kimatukio  baina ya wababe wawili waliosababisha  mauaji makubwa na udhalilishaji wa kutisha katika  kitatange kinachoendelea nchini humo.

Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com
Katika kutafakari mambo na hali inavyoendelea nchini Irak,safu hii imeonelea ijaribu kutoa mpambano wa kimatukio  baina ya wababe wawili waliosababisha  mauaji makubwa na udhalilishaji wa kutisha katika  kitatange kinachoendelea nchini humo.
 
Tujiulize kwa sasa hali nchini Iraki ikoje? Hakuna ubishi kuwa taifa hili lililowahi kuwa miongoni mwa mataifa ya kiarabu yenye nguvu za kisiasa na kiuchumi kwa sasa liko taabani tena  njia panda kuelekea kusambaratika kama juhudi za haraka kukomesha maangamizi yanayoendela hazitafanyika.
 
Uchumi,miundo mbinu,mifumo ya kiutawala na mshikamano wa wairaki kama wairaki vimevurugwa kiasi cha kutorekebika haraka. Iraki inavuja kiasi cha kukaribia kukata roho. Imejeruhiwa vibaya na tamaa za watawala wa magharibi kutaka kukandamiza na hatimaye kuzinyonya nchi za kiarabu.
 
Katika kuangalia mambo yalivyo Iraki ili tutafute ufumbuzi,safu hii leo imeamua kuwapambanisha Rais wa zamani wa Iraki,Saddam Hussein el Majjid na Rais wa Marekani, George W. Bush ili dunia iweze kutoa hukumu ya haki dhidi ya ni nani wa kulaumiwa hata kuhukumiwa siku moja kwenye mahakama ya kimataifa ya The Hague kule Uholanzi kama ilivyotokea kwa Charles Taylor,dikteta wa zamani wa Liberia.

Pia kama inavyopaswa kutokea kwa madikteta wengine kama vile Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni,( Uganda), Yahaya Jammeh, (Gambia),Albert Omari Bongo Ondimba, (Gabon), Denis Sassou Ngwesso, (Congo Braza),Blaise Compaore (Bukinabe),Meles Zenawi (Ethiopia) na wengine wenye sura na rangi zote za udikteta.

Ifuatayo ni orodha ya makosa ya Bush na Saddam:
 
Mauaji.
 
Mpaka sasa tunaambiwa kuwa Saddam anashikiliwa kizimbani kwa kuamrisha mauaji  ya wakurdi  maarufu kama mauaji ya Dujaila, ambapo mashia zaidi ya 100 waliuawa baada ya jaribio lao la kumuua Saddam kushindwa.
 
Hawa walizikwa kwenye kaburi la pamoja kwa mujibu wa Marekani. Jambo la kusikitisha hadi sasa hatuambiwi Marekani chini ya amri za Bush imeua wairaki wangapi ili tulinganishe na wale aliowaua Saddam.
 
Pia Saddam ikumbukwe aliwaua wakwe zake wawili kwa kosa la kumsaliti na kukimbilia Syria sawa na Bush alivyoamrisha kuuawa kwa watoto wawili wa Saddam waliokuwa wamekataa kujisalimisha.
 
Saddam aliua kwenye kijiji kimoja tu. Nalo hili halijawa kosa hadi mahakama ya haki (siyo hizi Kangaroo courts za kutengenezwa na Marekani), imkute na hatia.
 
Lakini ni ukweli usiopingika kuwa Bush ameua wengi kwa idadi na watokako.  Na siyo wairaki tu aliowaua Bwana huyu. Kwani majeshi kutoka Marekani, Uingereza , Poland na nchi nyingine yamo yanateketeza watu na kuteketezwa nchini Iraki. Jinai kama hii inaendelea nchini Afghanistan hata ukanda wa Gaza huku Lebanon ikiwa imepumua kidogo.
 
Utesaji.
 
Saddam ameshutumiwa kwa utesaji wa raia wake. Hatujaambiwa ni wangapi aliwatesa hadi sasa. Ila dunia inajua jinsi wanajeshi wa Marekani walivyotesa,kudhalilisha na hata kuua baada ya kubaka huko Iraki. Nani amesahau kuwa Saddam alijenga gereza la Abu Ghuraib na Bush akalitumia kutesea watu wasio na hatia?

Bush pia anahusishwa na mateso wanayoyapata watu wa Afghanistan , Lebanon na hata Cuba .  Hivyo ukiangalia kwa karibu unakuta kuwa makosa ya Bush yanafanyika kwenye eneo kubwa kuliko lile la hasimu wake Saddam.

 
Kupindua serikali.
 
Wakati Saddam anakabiliwa na shitaka la kupindua serikali moja, Bush anakabiliwa na makosa mengi juu ya hili. Kwani licha ya kupindua matokeo nchini mwake kwenye uchaguzi tata uliomuingiza madarakani,Bush anashitakiwa kwa makosa ya kupindua serikali za Iraki na Afghanistan huku akiwa anakula njama za kupindua serikali za Korea Kaskazini, Palestina , Lebanon , Cuba na Iran .
 
Kusababisha vifo na machafuko.
 
Wakati Saddam hana shutuma dhidi yake kwa kusababisha machafuko,Bush anakabiliwa na mashitaka mengi ya kuanzisha na kusababisha machafuko katika nchi nne kwa mpigo. Nchini Iraki ambapo mapambano ya mashia dhidi ya masunni yanaendelea kutafuna maelfu kwa maelfu,nchini Lebanon ,Palestina na Afghanistan .

Katika hili Saddam anasifiwa kuwa kusimamia mshikamano wa taifa kiasi cha kutawala muda wake wote bila kuwa na tatizo la vita baina ya mashia na masunni wala ghasia zisizokuwa na sababu.
 
Kusema uongo.
 
Katika jinai hii kuna ushahidi usiopingika kuwa Rais Bush aliudanganya ulimwengu kuwa Saddam alikuwa na silaha za maangamizi (Weapons of Mass Destruction- WMD) na pia alikuwa na uhusiano na kundi la Al-Qaeda na alishiriki kwenye mashambulio ya Septemba kumi na moja kwenye miji ya New-York na Washington.
 
Saddam kwa nguvu zake zote alikanusha kutokuwa na silaha hizi. Baada ya kupinduliwa imefahamika kuwa ni kweli Saddam maskini hakuwa na silaha hizo wala uhusiano na Al-Qaeda kama alivyodai Bush na CIA. Hivyo Bush aliidanganya dunia juu ya hili ili apate kisingizio cha kuhalalisha jinai yake ya kumpindua Saddam na kuivuruga nchi hii.
 
Wapelelezi wamejiridhisha kuwa hakuna silaha za maangamizi hata ya inzi wacha maangamizi ya umma,vinginevyo Bush azipeleke huko kipindi hiki anachoikalia Iraki.
 
Wapelelezi wanasema kuwa wamegundua njama za Bush kurudia jinai hii maana ni mkosaji mzoefu. Inasemekana kuwa anapanga uongo huu huu ili azivamie na hatimaye kusambaratisha tawala za Iran na Korea ya kaskazini.
 
Udikteta.
 
Wakati Saddam akisifika kufanya udikteta na ukandamiza  nchini Iraki  mwake tu, lakini Bush tofauti naye anasifika kuifanyia dunia nzima unyama huu. Nani mara hii kasahau maneno yake muda mchache baada ya kutokea kwa mashambulizi ya Septemba 11,2001? Alisema kuwa katika kuelekea vita ya ugaidi ni mawili,kumuunga mkono yeye au kutofanya hivyo uhesabike uko na adui yake!
 
Kuna kosa jingine hapa ambalo nalo laweza kuongezewa kwenye idadi ya makosa yanayomkabili Bush. Nalo ni kutumia njia za kigaidi kupambana na ugaidi.
 
 Katika kujitetea inasemekana kuwa Saddam atataka ushahidi wa kuwepo amani na mshikamano wakati wa utawala wake uletwe. Bush hapa hana chake maana wapiganaji wa kujitoa mhanga wameisambaratisha nchi.
 
Uzembe.
 
Wakati Saddam akikabiliwa shitaka la woga na  kuikimbia nchi na kujificha shimoni wakati nchi ilikuwa ndiyo inavamiwa,Bush  naye anakabiliwa na kosa hilo hilo alilolitenda siku ya tarehe 11 kuamkia 12 Septemba pale alipofichwa kwenye mashimo ya Colorado ili asishambuliwe badala ya kukimbilia kwenye eneo la tukio kama alivyofanya mtangulizi wake,Bill Clinton.
 
Wakati Saddam akikabiliwa na kosa la matumizi mabaya ya fedha ya umma,Bush hapa ndiyo kabisa ana zigo la lawama na makosa. Kwani amri zake zimeiletea dunia nzima hasara wakati Saddam aliisababishia Iraki peke yake.
 
Wakati ikisubiri kuona nini utakuwa mwisho wa unyama na ugaidi wa Marekani kwenye nchi nyingine kosa ambalo siku moja litamsimamisha Bush kule The Hague,ni vizuri dunia ya wapenda haki na amani ikawahukumu wababe hawa wawili.
 
Katika kusikikiliza kesi hii maarufu, mashahidi wawili wataitwa kutoa ushahidi juu ya hali halisi nao ni Rais Hugo  Chavez wa Venezuela na Rais Mahamoud Ahamadnajad wa Iran.
 
Kwa ufupi mnyambulisho tuliyoutoa,hatuna shaka kuwa kumbe hata mashetani wanazidiana.