KAMPUNI ya Wawekezaji ya Tanzanite One, imesema filamu ya watumwa wa vito ambayo inaonyesha utumikishwaji watoto katika madini ya Tanzanite Mererani, haitavuruga bei ya madini hayo.
Rais wa kampuni hiyo ambayo inajihusisha na uchimbaji wa madini ya tanzanite Mererani, Ian Harebottle, alisema kuwa ingawa filamu hiyo ina madhara katika soko la madini hayo, lakini kwa kuwa tanzanite inatoka Tanzania pekee, itakuwa ni vigumu kuvuruga bei.
"Bado thamani ya madini haya ipo juu, hivyo kuiporomosha kwa haraka katika soko la madini hayo kimataifa si rahisi kwani pia tayari tumetangaza sana madini haya, " alisema Harebottle.
Aliongeza kusema kuwa ,waandaaji wa filamu hiyo pia walifika katika eneo lao la kitalu C katika machimbo hayo lakini hawakuwapa ushirikiano wa kutosha kutokana na kutojua lengo hasa la filamu hiyo.
Hata hivyo, alisema kampuni yake kupitia taasisi yake ya Tanzanite Foundation imekuwa na mikakati mingine ya kutangaza madini hayo nje ya nchi.
Harebottle alisema hivi sasa nchi mbali mbali duniani zimekuwa zikinunua madini hayo kwa ajili ya kutengeneza vito na kwa shughuli nyingine tofauti na miaka ya nyuma.
Filamu la Utumwa wa vito ambayo inaonesha utumikishwaji watoto katika migodi ya madini ya Tanzanite Mererani iliyoandaliwa na Shirika la Habari la Kimataifa lilisilo la kiserikali la IRIN imezinduliwa hivi karibuni nchini Marekani