Chavez amuita Bush shetani.
Jana tarehe 19 Septemba, marais wa Marekani George W. Bush na mwenzake wa Iran, Mahamoud Ahamadnajad, walihutubia mkutano wa baraza la umoja wa mataifa jijini New -York.
Pamoja na kuwa kikao hicho kinahudhuriwa karibu na viongozi wote wa dunia,ni watu hawa wawili hawa ambao ni mahasimu wakubwa, ambao ni sawa na Daudi na Goliati,waliovutia watazamaji karibu dunia nzima.
Bush alikuwa wa kwanza kuhutubia majira ya asubuhi huku Ahamadnajad akifanya hivyo usiku.
Kutokana na uhasama wa marais hawa wawili, wanaitifaki wa umoja wa mataifa na Marekani, walipata kibarua kigumu kuwaweka chini ya paa moja.
Kila mmoja alijitahidi kupata sababu ya kumkwepa mwenzake. Kwa mfano, Rais wa Iran alikataa kuhudhuria wakati wa hotuba ya Bush kwa kisingizio kuwa kulikuwa kunagawiwa pombe wakati Bush hakuhudhuria wala hakutoa sababu.
Katika hotuba ya Bush aliishutumu Iran kama kawaida yake na kuisihi iachane na mipango yake ya kurutubisha urania kwa ajili ya kutengeneza bomu la nyuklia shutuma zilizokanushwa na Iran baadaye.
Pia Bush alitumia nafasi hiyo kuongea na sehemu mbali mbali zilizomo kwenye migogoro kama vile Lebanon, Palestina, Darfur, Afghanistani na Irak. Hotuba yake ilikuwa fupi na tofauti na zile zilizozoeleka. Kwani haikuwa na ukali na vitisho.
Kwa upande wake Ahmedinajad aliyejizoelea sifa za kuwa kiongozi pekee kutoka nchi changa kumkalia kidedea Bush pamoja na umoja wa mataifa kwa ujumla, aliwaacha hoi wachambuzi kwa kutoa hotuba iliyokuwa ya kidiplomasia tofauti na alivyokuwa akitegemewa kufanya.
Wachambuzi wanasema kuwa kwenye mpambano huu Ahamadnejad alimshinda Bush.
Kwanza kutokana na maneno aliyotumia kwenye hotuba yake kuonyesha kuwa kwa sasa amebadili jukwaa na kuwa mtetezi wa nchi zinazoendelea na mpenda na mtetezi wa haki.
Pili "timing" ya hotuba yake. Kitendo cha kuweza kuushawishi umoja wa mataifa akahutubia siku moja tena baada ya hasimu wake kilielezewa kama kujua kuchanga Karata zake vizuri. Hata ile hali ya kupangiwa kuhutubia jioni ilionyesha kuwa kama kete ya kupata kuangaliwa na watazamaji wengi hasa wa Marekani.
Anderson Cooper, mtangazaji wa kipindi cha Anderson Cooper 360 alisema wazi wazi kuwa Karata alizocheza Ahmadnejad zimeonyesha ukomavu wa kisiasa na kumpiku hasimu wake Bush.
Pia mshauri wa zamani wa Rais wa masuala ya ulinzi na kigeni wa Marekani, Zbignev Brewzski na Balozi wa zamani wa Marekani kwenye umoja wa mataifa, Richard Hallbrooke waliishangaa na kuilaumu wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani hata Bush kukubali kushindwa kirahisi hivi.
Katika hotuba yake, Ahmadnejad, iliyoshangiliwa sana baada ya kumalizika huku ikiwa inasikilizwa kwa makini, alibainisha mambo makuu mawili yaani silaha za nyukilia na ubabe unaosababisha kuvunja haki za dunia kunakofanywa na mataifa makubwa.
Marais vikaka kama vile Rais wa Ufaransa, Jaques Chirac hawakusikika sana kama mahasimu wawili Bush na Ahamadnajad.
Alishangaa ni kwa jinsi gani haki inaweza kupatikana kwenye umoja wa mataifa ambapo wahalifu wenye historia mbaya ya matumizi ya dhana za nyukilia wana uanachama wa kudumu unaowapa turufu! Japo aliilenga Marekani na mshirika wake Israel, hakutaja nchi kwa jina.
Alidai afrika, umoja wa nchi za kiislamu na umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote zipewe viti vya kudumu kwenye baraza kuu la umoja wa mataifa na ziwe na kura ya turufu ili kuweza kupambana na uhalifu unaoendelea ambao unatishia mstakabali wa dunia kwa ujumla.
Ahamadnejad alilaani ukaliwaji wa nchi moja unaofanywa na nchi nyingine kwa kisingizio cha kueneza demokrasia. Pia aliushutumu umoja wa mataifa kwa kutokuwa na nguvu mbele ya mataifa makubwa. Alitoa mfano wa Lebanon ambapo Umoja wa Mataifa ulishindwa kusitisha vita. Aliuambia wazi wazi kuwa unaburuzwa na nchi tajiri hasa Uingereza na Marekani.
Pia alilaani njama za mataifa makubwa kutotaka nchi nyingine ziwe na vinu vya kiraia vya kinyuklia wakati zenyewe zimejilimbikizia maelfu na matani ya silaha za maangamizi ya halaiki.
Kilichofanyika kwenye mkutano wa umoja wa mataifa ni sawa na mpambano wa Daudi na Goliati.
Kimsingi amefuta utamaduni wa unafiki na woga wa kuogopa kuwaambia watawala wa Marekani kuwa ni wahalifu tena nchini mwao.
Kwa sasa Ahamadnajad amejitokeza kuwa msemaji wa ulimwengu wa kiislamu na nchi zinazoendelea akiwa anaungwa mkono na wakongwe kama Fidel Castro wa Cuba, Hugo Chavez wa Venezuela na hata Kim Jong-Il wa Korea ya Kaskazini.
Wakati Ahamadnajad akijizoelea sifa ya kumsema Bush ndani ya nchi yake, Rais Hugo Chavez wa Venezuela alitoa mpya. Kwani licha ya kuishutumu na kuishambulia Marekani, alimwita Rais George W. Bush shetani.
Alinukuliwa akisema "Jana shetani alikuwa hapa (Kwenye jukwaa alipokuwa akihutubia),alikuwa hapa na bado pananuka salfa-Sulphur"
Baada ya kusema maneno hayo alifanya alama ya msalaba na kuendelea na hotuba yake ambayo kimsingi ilijaa lugha kavu ya moja kwa moja na isiyo ya kidiplomasia.