RAIS wa Marekani, George Bush na wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, walitarajia kuhudhuria Mkutano Mkuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) huku wakiripotiwa kwamba watafanya kila linalowezekana wasikutane ana kwa ana.
Bush amepangiwa kuhutubia mkutano huo kwenye makao makuu ya UN huku Ahmadinejad akihudhuria.
Ahmadinejad ni mkosoaji mkubwa wa sera za kigeni za Marekani na ambaye hivi karibuni alimtaka Bush washiriki katika mjadala.
“Nina uhakika wote wawili watafanya kila linalowezekana kukwepana,” Naibu Katibu Mkuu wa UN, Mark Malloch Brown, alisema.
Marekani inaituhumu Iran kuitumia programu yake ya nyuklia kutaka kutengeneza silaha za nyuklia, huku Teheran ikisisitiza kwamba programu yake ni kwa madhumuni ya amani.
Baraza la Usalama la UN liliitaka Iran isitishe urutubishaji wa madini ya uranium ifikapo Agosti 31 ama ikabiliane na uwezekano wa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi.
Iran ilipuuza tarehe hiyo lakini ilisema kwamba itafikiria kusitisha kwa muda kama masharti ya kuanza mazungumzo na Marekani.
Urutubishaji wa uranium ni hatua muhimu ya utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Mwezi uliopita, Ahmadinejad alitoa changamoto kwa Bush kushiriki katika mjadala wa televisheni ili Iran iweze kueleza jinsi ya kumaliza matatizo yanayoikabili dunia.
Ikulu ya Marekani ilitupilia mbali ofa hiyo ikisema kuwa ni ujanja wa kutaka kupoza suala la mzozo wa nyuklia.
Ijumaa iliyopita, alipoulizwa iwapo atakutana na Ahmadinejad, Bush alijibu: “Hapana, Sina mpango wa kukutana naye. Nimeshaweka wazi kwa utawala wa Iran kwamba tutakaa nao pale watakapositisha urutubishaji wa uranium, na ninashikilia msimamo wangu.”
Bush anategemea wakati wa hotuba yake katika mkutano huo kuwataka wanachama wa UN wachukue hatua zaidi katika harakati za kupambana na udhalimu hususan Mashariki ya Kati, mshauri wa masuala ya usalama wa taifa, Stephen Hadley, alisema juzi.
Akigusia yaliyomo katika hotuba hiyo, Hadley alisema Bush atajadili juhudi za kujenga demokrasia Mashariki ya Kati, akitumia kile kinachojulikana kama ajenda ya uhuru yenye kuwapa watu mwanga na maono ya matumaini na fursa nzuri kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
CNN