Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Chavez, Ahmadinejad waishambulia Marekani
http://www.habaritanzania.com/articles/1052/1/Chavez,-Ahmadinejad-waishambulia-Marekani
By Manyerere Jackton
Published on 09/20/2006
 
VIONGOZI wanachama wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), waliokutana mjini hapa, walizishambulia sera mbaya za Marekani dhidi ya mataifa yanayoendelea.

Na Manyerere Jackton, Havana, CUBA

VIONGOZI wanachama wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), waliokutana mjini hapa, walizishambulia sera mbaya za Marekani dhidi ya mataifa yanayoendelea.

Wakihutubia wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa 14 wa NAM, viongozi hao walisema wakati umefika sasa wa kuwa na usawa katika masuala ya biashara na mengine ya kijamii.

Rais wa Venezuela, Hugo Chavez, alikuwa mwiba mkali kwa Marekani, baada ya kuishambuli wazi wazi kutokana na kile alichokiita uonevu kwa mataifa yanayopingana na sera zake.

Katika kuonyesha kukerwa na sera za taifa hilo, Chavez aliweka kando hotuba yake iliyoandikwa kwa lugha ya kidiplomasia, na kuanza kuzungumza kwa maneno makali. Wajumbe walimshangilia muda wote.

“Cuba ni kielelezo cha uvumilivu wa sera za Marekani, Cuba imetupa somo zuri, na sisi Venezuela tunaiga mfano wao, NAM sasa inaingia katika zama mpya.

“Naamini kuwa chini ya uongozi wa Fidel Castro, NAM sasa inaingia katika zama mpya, sisi wa Kusini tunataka kuishi kwa haki sawa kama walivyo wa Kaskazini, hatutaki kuonewa-tutashinda,” alisema Chavez.

Kabla yake, alizungumza Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad. Alishambulia sera za Marekani na kusema nchi za Kusini lazima sasa ziungane ili kujenga umoja wenye nguvu zaidi.

“Miaka 45 ya NAM, sasa kuna umuhimu wa kuimarisha umoja zaidi kuliko hapo awali,” alisema kiongozi huyo hasimu wa Marekani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa (UN), anayemaliza muda wake, Kofi Annan, akitoa salamu zake, alitoa wito kwa mataifa kuheshimu haki za binadamu, demokrasi, haki za watoto wa kike na wanawake, uhuru wa vyombo vya habari na kadhalika.

Alitoa wito pia kwa serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, akitilia mkazo vita dhidi ya umaskini na mgawo sahihi wa rasilimali za taifa.

Annan alisema ni jambo muhimu kwa maliasili za taifa, kuwanufaisha wananchi wote, badala ya kunufaisha kikundi cha wateule wachache.

Rais Kikwete alihutubia mkutano huo kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.