CHAMA cha Wafanyakazi wa Utalii, Hoteli na Majumbani, kimesema wawekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar wamekuwa wakikataa kufunguliwa matawi ya vyama vya wafanyakazi katika miradi yao.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ali Salum Ali, katika kikao kilichowakutanisha Kamisheni ya Kazi Zanzibar, chama hicho cha wafanyakazi pamoja na Chama cha Waajiri (ZANEMA).
Ali alisema kwamba wawekezaji wengi katika hoteli za kitalii wamekuwa wakilalamikiwa kulipa masilahi madogo wafanyakazi na hakuna chombo cha kuwatetea kwa vile hakuna matawi ya wafanyakazi.
Alieleza kwamba pamoja na Zanzibar kuwa na idadi kubwa ya hoteli za kitalii, lakini hadi sasa ni chache zilizoruhusu matawi ya wafanyakazi kuwapo, na wengine wanatishia kuwafukuza kazi wale watakaofungua matawi hayo katika sehemu zao za kazi.
Alizitaja hoteli zilizofungua matawi ya wafanyakazi hadi sasa kuwa ni Sea Club, Bravo Hotel, La Gema Hotel, Coral Reef Hoteli, Pongwe Beach, Coco De Mer Hotel, Tembo Hotel, Mazson Hotel na Dhow Palace.
Alisema hoteli nyingine zilizosalia hazina matawi ya wafanyakazi na menejimenti zimeendelea kuvunja sheria kwa kuwafungisha mikataba ya muda mfupi wafanyakazi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za wafanyakazi.
“Kuanzia sasa tutafungua mashitaka kwa hoteli zote Mahakama ya Kazi, ili kuona wafanyakazi katika hoteli wanapata haki ya kuwa na vyama katika sehemu zao,” alisema.
Alieleza kwamba miongoni mwa malalamiko mengi ya wafanyakazi katika sekta hiyo ni kuwa wanafungishwa mikataba ya miezi mitatu, hivyo kushindwa kunufaika na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambao unataka mwanachama kuanza kunufaika nao baada ya kuchangia kwa muda wa miaka mitano.
Alisema kwamba wafanyakazi hao wamekuwa hawalipwi fedha za usafiri, likizo, matibabu, kodi ya nyumba pamoja na malipo ya kufanya kazi katika muda wa ziada.
“Wanakuja kulalamika kwetu kutokana na Kamisheni ya Kazi kudaiwa inashindwa kuwachukulia hatua za kisheria wawekezaji wanaovunja sheria,” alisema.
Aidha, alisema kwamba wafanyakazi katika hoteli za kitalii Zanzibar wamekuwa wakilalamika kwamba wafanyakazi wa kigeni wamekuwa wakilipwa mishahara mikubwa kulinganisha na wale wazalendo licha ya kuwa na viwango sawa vya taaluma.
Alitoa mfano kuwa ipo hoteli moja ya kimataifa inawalipa wahasibu wa kigeni zaidi ya sh milioni moja wakati wazalendo wanalipwa sh 300,000 pamoja na kuwa wote wana kiwango sawa cha elimu ya uhasibu.
Kikao hicho cha pamoja kimekuja baada ya Chama cha Waajiri Zanzibar (ZANEMA) kuwasilisha malalamiko Kamisheni ya Kazi wakikitaka Chama cha Wafanyakazi (ZATHOCODAWU), kizuiwe kufungua mashitaka mahakamani dhidi ya waajiri kabla kesi zao kupitia Kamisheni ya Kazi.
Hata hivyo, Kamishna wa Kazi, Iddi Ramadhana Mapuri, alisema kwamba malalamiko hayo hayana msingi wowote kwa vile haki ya kwenda mahakamani ni ya kikatiba kwa mtu au taasisi yoyote.
Alizitaka pande zote kuhakikisha zinazingatia sheria za kazi ili kuondosha malalamiko ambayo yanajitokeza kuwa wafanyakazi wamekuwa hawatendewi haki kutokana na sheria za kazi kutozingatiwa.