UONGOZI wa Benki ya National Microfinance (NMB), umeanza kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazotolewa na wateja wa benki hiyo kuwa, wanakatwa fedha zao kinyume cha utaratibu uliowekwa.
Hatua hiyo inachukuliwa baada ya kuwapo tuhuma za wateja kwenye mikoa ambayo NMB ina matawi, kwamba hukatwa fedha zao kwa muda mrefu sasa bila kupewa taarifa.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake jana, Meneja Uhusiano wa NMB, Shy-Rose Bhanji, alisema endapo ikibainika, wanaohusika watachukuliwa hatua za kisheria.
“Tumeanza kufanya uchunguzi mara moja baada ya kupokea tuhuma hizi kuhusu wateja wetu ambao wamekuwa mhimili mkubwa kwetu, sasa kama atabainika mfanyakazi yeyote, atachukuliwa hatua kali,” alisema Bhanji.
Aliwataka wananchi ambao wamekuwa wakikatwa fedha zao kinyume cha sheria, kutoa taarifa hizo makao makuu au kwenye matawi yaliyopo karibu nao ili madai hayo yashughulikiwe.
Alisema taarifa zote zitakazotolewa zitapokewa kwa siri ili kutatua tatizo ambalo linaonekana kutaka kuipaka matope benki hiyo.
Mkoa ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu ni Mara, ambako walimu kutoka shule mbalimbali za msingi wamekuwa wakidai kukatwa fedha zao kinyume cha utaratibu.