KANISA Katoliki nchini, kupitia Baraza la Maaskofu (TEC), litatoa tamko lake rasmi kuhusu hoja ya kutaka kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Novemba mwaka huu.
Mwenyekiti wa TEC, Askofu Yuda Thadei Ruwa’ichi, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Dodoma, alithibitisha hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Walei ya Jimbo la Dodoma uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Vijana, Parokia ya Kiwanja cha Ndege mjini hapa.
Askofu huyo, alisema kanisa halijawahi kutoa tamko lake rasmi, ingawaje kwa nyakati tofauti limewahi kuzungumzia suala hilo mara tatu.
Akieleza zaidi, alisema kwa mara ya kwanza, Februari mwaka huu, TEC ilimwomba Rais Jakaya Kikwete atazame masuala mbalimbali nchini, ikiwamo hoja ya kutaka kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Mara ya pili, Juni mwaka huu, kanisa lilirudia kumwomba Rais Kikwete aangalie haja ya kutazama upya masuala mbalimbali nchini, likiwamo tena la hoja ya kutaka kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini.
Askofu Ruwa’ichi aliongeza kuwa, Kanisa hilo lilizungumzia tena suala hilo Agosti mwaka huu, pale waandishi wa habari walipowahoji makatibu wa baraza hilo.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema kuwa TEC inaukataa msimamo wowote ule ambao unaweza kuleta mpasuko na kuvuruga amani na umoja wa kitaifa wa Watanzania.
Alieleza kuwa, TEC haina matatizo yoyote kwa Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi kama dini yao inavyoagiza, lakini akaonya kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima iheshimiwe, hasa kwa kuzingatia kuwa serikali hii haina dini.
Akizungumza na wajumbe hao waliowakilisha Wakatoliki wapatao 350,000 wa jimbo hilo, Askofu Ruwa’ichi alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira si ya kiroho tu ambayo ni ya ndani, bali hata yanayowazunguka ili yazidi kuwafaa na vizazi vijavyo.
Alisema kwa kuzingatia kilimo bora na hifadhi nzuri ya mazingira, Mkoa wa Dodoma unaweza kuepukana kabisa na sifa ya kuitwa mkoa wenye ukame.
Aliwahimiza wajumbe hao kusoma na kuizingatia kwa makini hotuba ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, kuhusu mazingira nchini na kuwafikishia waumini wao kwenye parokia zote 36 jimboni humu.
Aidha, wakati jimbo hili linaelekea kuadhimisha miaka 100 tangu Ukatoliki ulipoingia Septemba mwakani, askofu huyo amewahimiza waumini wake kuimarisha uadilifu na uhusiano mwema kati yao na binadamu wengine na pia uhusiano mwema kati yao na Mungu.