Bei ya mafuta, yaani petroli imekuwa haina msimamo katika soko la dunia na kuwa ni jambo linaloziumiza nchi nyingi zinazoagiza mafuta hayo kutoka nchi zinazozalisha kwa wingi, hususan kutoka Mashariki ya Kati. Ili kuepuka utegemezi huo umekuwapo msukumo wa kutafuta mbadala wa mafuta hayo. MWANDISHI WETU anafahamisha zaidi katika makala hii.
WAKATI bei ya mafuta ikiwa inapanda na akiba ya mafuta duniani ikiwa inapungua, njia mbadala imekuwa kutafuta nishati hiyo kutoka kwenye mimea hususan mihogo, miwa na mibono ambayo inaonyesha mafanikio na inaweza kuwa mbadala wa mafuta asilia kwa kiwango cha kati ya asilimia kumi na asilimia 25 ya petroli kwa magari yenye injini za kawaida na hadi asilimia 100 kwa injini zilizofanyiwa marekebisho.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), shinikizo linalotokana na kupanda kwa bei ya mafuta sanjari na haja ya kutunza na kuhifadhi mazingira, nguvu zimekuwa zinakusanywa na kuelekezwa kutafuta mbadala kutoka kwenye mazingira yake, yaani baio-nishati kutoka mimea mbalimbali ikiwamo miwa, mbegu za mafuta kama alizeti na ufuta.
Aidha, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika hilo, Idara ya Maendeleo Endelevu, Alexander Muller, Aprili mwaka huu 2006 alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 15 na 20 ijayo jamii inaweza kuwa na dizeli au kupata nishati ya mafuta yanayotokana na mimea kwa kiasi cha asilimia 25 ya nishati inayohitajika duniani.
Naye Mratibu Mwandamizi wa Nishati wa shirika hilo, Gustav Best, anasema kuwa angalau kwa kiasi fulani inaonyesha kuwa unakuwapo mwamko mpya wa maisha kwa bidhaa mbalimbali kama sukari, ambazo bei yake imekuwa inayumba.
Brazil ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa mafuta yanayotokana na mimea kwa kuzalisha hekta-lita milioni 120 kwa mwaka kutoka kwenye miwa na mihogo. Katika nchi za Thailand na China miradi kadhaa ya kuzalisha mafuta yanayotokana na mihogo kwa matumizi ya viwandani ipo njiani.
Wazo la kutumia dizeli inayotokana na mimea lilianza wakati tatizo la mafuta lilipotokea mara mbili katika miaka ya 1970, hivyo kwamba nchi kadhaa hazikusubiri hadi yafikie kiwango kikubwa cha bei za mafuta kilichopo sasa na badala yake zilianza kutafuta njia mbadala za kukabiliana na tatizo hilo.
Nchini Brazili magari yote yanatumia mafuta yaliyochanganywa kwa asilimia 25 na dizeli inayotokana na miwa ikiwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kutumia dizeli hiyo ya ‘kijani’ hivi sasa inazalisha lita bilioni 12 kwa mwaka, kiwango ambacho kinakaribia theluthi moja ya mafuta yanayozalishwa duniani ambacho ni lita bilioni 35. Hali kadhalika gharama ya dizeli ya mimea kutoka Brazil ni dola 25 kwa pipa, ikiwa ni takriban nusu ya bei ya mafuta asilia.
Afrika Kusini kwa upande wake ilianza kutumia nishati inayotokana na mimea kwenye viwanda wakati wa utawala wa kibaguzi, ikiwa ni kukabiliana na vikwazo vya biashara na kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya utawala huo na moja ya kizuizi kilikuwa ni kutouziwa mafuta.
Hivi sasa dizeli ya mimea nchini humo inazalishwa na Shirika la Maendeleo ya Nishati (EDC) ambalo hununua mahindi ya ziada kutoka kwa wakulima na kuyatumia kutengeneza mafuta, ambapo tani milioni tatu za mahindi huzalisha lita bilioni 1.26 za mafuta, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 12 ya mahitaji ya nishati kwa Afrika Kusini, pia hutumia miwa na uwele kutengeneza mafuta.
Dhahabu ya kijani au nyeusi
Kwa upande mwingine nchi nyingi za Afrika zimeshuhudia gharama za mafuta zikipanda, hata hivyo zipo nchi chache zinazozalisha mafuta lakini hulazimika kuuza mafuta yasiyosafishwa na kuagiza mafuta yaliyosafishwa. Nigeria ni mfano hai ambapo huzalisha takriban mapipa milioni mbili ya mafuta yasiyosafishwa kwa siku na huyategemea kwa asilimia 90 kupata fedha za kigeni.
Mwanzoni mwa mwaka huu 2006, Nigeria ilitarajiwa kupitisha sheria ya kuidhinisha matumizi ya asilimia kumi ya baio-nishati kwenye petroli, hivyo kupunguza kiasi cha fedha zinazotumika kwenye mafuta, pia kiwango cha uchafuzi. Katika kipindi kifupi mafuta hayo yanayotokana na mimea yatakuwa yanaagizwa kutoka Brazil lakini katika malengo ya muda mrefu yatakuwa yanazalishwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Jarida la Oil and Gas, ‘Dizeli kijani’ kama njia mbadala inaonekana ndio muafaka ya kuokoa kiasi cha rasilimali ya mafuta kilichobakia ardhini ambacho kinakadiriwa kufikia tani bilioni 140 sawa na mapipa katika kipimo cha jiga (giga) 1,050.
Hali kadhalika kwa mujibu wa US Geological Survey, kiasi cha rasilimali ya mafuta kilichobakia ni sawa na tani bilioni 160, sawa na mapipa kwa kipimo cha jiga 1,200.
Aidha, Shirika la Maendeleo na Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) linatahadharisha kuwa iwapo kiwango cha uzalishaji na utumiaji wa mafuta kitaendelea kama ilivyo sasa, basi akiba ya mafuta iliyopo duniani itakuwa imekwisha katika kipindi kisichozidi miaka 65 kuanzia sasa.
Kuanzia mwaka 1997 nchi nyingi chini ya Protokali ya Kyoto ziliridhia kupunguza uchafuzi wa hewa hususan inayotoka viwandani kwa angalau asilimia tano chini ya kiwango cha mwaka 1990 na lengo hilo liwe limefikiwa kati ya mwaka 2008 na 2012.
Tofauti na petroli ambayo huzalisha kaboni ambayo awali huwa imehifadhiwa ardhini na kuingia angani, dizeli inayotokana na mimea hutoa kaboni inayotoka angani ambayo inapoungua hurudi kwenye makazi yake ya asili.
Kituo cha Kimataifa cha Utafiti kwa Maendeleo (CIRAD) kimekokotoa kuwa ‘dizeli kijani’ itatumika na kuwa mbadala wa mafuta ya kawaida kama bei za mafuta hayo zitaendelea kuwa juu kufikia angalau (dola 70 hadi 80 kwa pipa).
Tatizo jingine linaegemea kiwango cha matumizi ya mwaka 2004, ambapo inatakiwa kuilima ardhi kwa takriban mara sita zaidi ili kufikia au kuwa na kiwango kinachotosha kuwa mbadala wa mafuta asilia.
Katika eneo la Caribbean na St Kitts ambako viwanda vya sukari vilifungwa Julai 2005, wanaangalia mapendekezo yaliyotolewa na kampuni za Norway na Marekani ya kushughulikia sehemu ya mazao ya miwa na mkakati huo utahusisha eneo la hekta 2,500 zinazolimwa miwa.
Guyana kwa upande wake Oktoba 2005 ilisaini mpango wa ubia na Brazil, na Jamaica inatarajiwa kufuata njia hiyo hiyo.
Mikakati mingine na tofauti, inalenga kuzalisha kuwaongezea kipato wakulima wadogo na kupata miwa mingine kwa ajili ya kutengeneza nishati itakayotumika kwenye vyombo vya usafiri na sekta ya umeme.
Nigeria imechagua kuzalisha dizeli hiyo kutoka kwenye mihogo. Sheria imepitishwa mwaka huu 2006 kuruhusu asilimia kumi ya dizeli inayotokana na mimea kuchanganywa na petroli ili kupunguza gharama ya mafuta na kiwango cha uchafuzi wa hali ya hewa kwa njia hiyo moja.
Katika hatua ya kwanza, mafuta yanayotokana na mimea yataagizwa kutoka Brazil. Mimea mingine ambayo inatoa matumaini ya kupatikana kwa umeme ni pamoja na uwele ambao hauhitaji mbolea nyingi na huvumilia ukame, na Jamhuri ya Dominica itazindua mtambo wa dizeli inayotokana na uwele ambao utafungwa kwenye njia ya kiwanda kinachotumia umeme wa Megawati 20.
Nchini Malawi wakulima wamekuwa wanahimizwa kulima miti ya mibono na waachane na kilimo cha tumbaku kutokana na kigezo kuwa miti hiyo inastahamili ukame, ni rahisi kuitunza na si rahisi kuliwa na wanyama, kwa kuwa hutoa harufu ambayo haivutii wanyama. Zaidi ya miti milioni moja imekwishaoteshwa nchini humo.
Nchini Mali, mpango wa taifa unaolenga nishati itakayotokana na mibono umepanga kutumia mmea huo kwa ajili ya kutoa nishati kwa maeneo ya vijijini na kwa ajili ya usafirishaji. Lengo ni kumudu kutoa umeme kwa vijiji 350 katika maeneo ya Kayes, Koulikoro, Segou na Sikasso kati ya mwaka huu na mwaka 2008.
Nchini Tanzania hivi karibuni Kampuni ya BMTL ilianzisha kampeni ya kupanda miti takriban 2,000 katika viwanja vya Shule ya Msingi Kawe B, jijini Dar es Salaam, miti aina ya mibono (Jatropha Curcus) na kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ketul Patel, kampuni hiyo iliamua kuchagua aina hiyo ikiwa inalenga kuokoa maisha na kuujenga uwiano ndani ya mfumo wa ekolojia.
Mibono ni miongoni mwa miti ambayo ina manufaa kadhaa kwamba ni pamoja na kuwa majani yake hayatumiwi au hayaliwi na wanyama na kwamba inaweza kuzalisha kuni na matunda yake yana asilimia 50 ya mafuta ambayo yanaweza kutumiwa kutengeneza mishumaa, sabuni na zaidi ya yote mbegu hizo zinaweza kutoa mafuta, yaani dizeli inayoweza kutumiwa na mashine mbalimbali au mafuta ya taa ambayo ni nishati muafaka kwa jamii za vijijini.
Miongoni mwa nchi ambazo zimewahi kufanikisha zoezi zima la kukamua mbegu za mafuta ya mibono hadi kufikia dizeli yenye ubora ni India ambapo mwanzoni mitambo mitatu katika eneo la Bhavnagar iliweza kuzalisha kiasi cha lita 100 kwa siku.
Ndani ya mitambo hiyo midogo mafuta ya mibono yalipitishwa na kuchujwa na hayana tofauti na dizeli inayopatikana kutoka kwenye mbegu nyingine za mafuta, ikiwamo maharage ya soya ambayo huzalisha dizeli hususan miongoni mwa nchi za Ulaya na Marekani.
Nchini India dizeli inayotokana na mafuta ya mibono imewahi kufanyiwa majaribio na kufikia hitimisho kuwa haina tofauti na aina nyingine za dizeli, hasa baada ya kufanya matengenezo au marekebisho kidogo kwenye injini ya gari lililotumika, Mercedes-Benz C 220 CDI ambalo liliweza kufanya safari ya kilometa 5,900 kati ya Aprili na Mei 2004, ikiwa ni pamoja na kupitia miji 11 mikubwa ikiwemo Pune, Bangalore, Hyderabad, Mumbai na Delhi.
Japo matumizi ya dizeli iliyotokana na mibono ilikuwa inafanyiwa majaribio, jaribio hilo lilifanikiwa kutokana na sababu mbili ; ya kwanza ni kubainisha kuwa mafuta yanayotokana na mibono yanaweza kutumiwa bila tatizo kwenye injini aina ya CDI zilizokarabatiwa ili ziweze kutumia baiodizeli. Hali kadhalika mafuta yanayozalishwa nusu ya haidrokaboni haikuunguzwa na theluthi moja ya haidrokaboni hiyo iliyozalishwa kutoka.
Sababu ya pili ni kuwa timu ya wataalamu nchini humo iliungwa mkono hivyo kwamba majimbo mengine mawili nchini humo yamejizatititi na kuanza kuotesha miti hiyo katika maeneo ambayo yanaonekana kuwa hayafai kwa kilimo.
Duniani kote majaribio yanafanywa kwa upana kuangalia namna ya kupata mafuta yatakayotumiwa kama nishati kutoka kwenye mimea yenye mbegu zinazotoa mafuta ikiwamo nazi, mchikichi, mbegu za pamba, alizeti, karanga, soya na mbegu zinazoingia katika kundi hilo ambazo zimekuwa zinatoa matumaini ya kuwa miongoni mwa vyanzo vya bei ya chini vya kupata mafuta ya mimea.
Hata hivyo si kila mtu anaamini kwenye uzalishaji wa nishati hiyo kutoka kwenye mimea. Yamekuwapo mawazo kinzani kwamba kujikita kwenye utafutaji wa nishati hiyo kutatoa shinikizo la mzigo kwa maeneo muhimu ya mfumo wa ekolojia, kutaathiri rutuba ya udongo na hata kusababisha kupungua kwa kiwango cha maji na hivyo kuishia kulazimisha au kuingiza matumizi ya mbolea za chumvichumvi na kemikali za kuulia wadudu.
Hali kadhalika zipo dhana kuwa wakati mafuta hayo yatakapokuwa yanaunguzwa kwa ujumla yatazalisha kiasi kidogo cha hewa ya monoksaidi ya kaboni, dayoksaidi ya salfa na nyingine zinazohusiana, na zitatoa kiwango kikubwa cha chembechembe zenye sumu.
Hata hivyo tathmini za nishati duniani zimekuwa zikitoa tathmini dhidi ya hoja hizo kinzani za nishati ya mimea. Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa Julai 2005 na watafiti wa Chuo Kikuu cha Berkeley nchini Marekani unadai kuwa kuzalisha soya kwa ajili ya nishati ya dizeli kunatumia asilimia 27 ya nguvu inayotumika kuzalisha petroli.
Utafiti unaainisha kuwa ushindani utakuwapo miongoni mwa nchi maskini katika uzalishaji wa mazao ya chakula na mazao ya nishati ya mafuta, jambo ambalo linazua mijadala kadhaa.
Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linaeleza kuwa kama uzalishaji wa nishati mbadala utaongezeka, mahitaji ya ardhi kwa ajili hiyo yatakuwa makubwa. Aidha, kiwango cha matumizi ya nishati ya mafuta yanayotokana na mimea kitawezesha kupima jinsi ardhi inavyotakiwa kutumiwa na hivyo kuongeza kwa haraka bei za vyakula miongoni mwa nchi maskini.
Kuelekea maendeleo safi
Ipo hatari ya kutowiana katika nchi ambazo mafuta hayo yatazalishwa kwa gharama nafuu na nchi ambazo mahitaji yake yanakua kwa haraka. Katika tukio lolote ni rahisi kushusha bei ya mafuta yanayotokana na mimea hivyo kwamba kila sehemu ya mimea inatumika, kama vile sehemu za mimea kama magome na taka nyingine zinazotokana na mbao.
Juni 2005, Shirika la Maendeleo ya Viwanda na Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) lilizindua mkakati wa mafuta yanayotokana na mimea. Kundi la wataalamu wa kimataifa liliundwa kusaidia nchi zinazoendelea kunufaika kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji, kutumia na kufanya biashara ya mafuta hayo. Mkakati huo umenuia kuanzisha uwekezaji mpya kupitia miundombinu safi ya maendeleo.
Aidha, Azimio la Doha lililoridhiwa na Shirika la Biashara Duniani (WTO) mwaka 2001, limejielekeza kwenye hali hiyo pia kwa kutoka msukumo wa majadiliano juu ya kupunguza au kuondoa ushuru na vikwazo visivyo vya ushuru kwa bidhaa na huduma za mazingira.
Baio-nishati inayopatikana kwenye uendeshaji wa kilimo endelevu itawezesha nchi zenye kipato cha chini na kati kuunda au kuanzisha soko la mauzo nje ya nchi. Azimio hilo linabainisha kuwa baio-nishati inaweza kuchochea uwepo mgawanyo ulio sawa wa uchumi duniani.
Ni dhahiri kuwa nishati mbadala itawezesha jamii maskini kumudu kuendesha gharama zao za maisha na kuepuka kigezo kikuu na kandamizi cha petroli, hususan kwa nchi ambazo hazijagundua rasilimali hiyo na ikiwa tafiti changa zilizopo zitapewa kipaumbele na kuboreshwa ili kufikia lengo.