Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waliodai Pemba hakuna njaa wawajibishwe
Waliodai Pemba hakuna njaa wawajibishwe
By Habari Tanzania | Published  09/19/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

KATIKA dunia ya leo ya utandawazi, kama walivyoeleza vizuri wanamuziki wa bendi ya Msondo Ngoma ya Dar es Salaam, ni muhimu kila jambo kuwekwa hadharani.

Hii ni kusema, huu si tena wakati wa kuficha jambo; liwe zuri au baya, kwa sababu kufanya hivyo hakumsaidii anayeficha wala anayefichiwa. Badala yake huwa na madhara makubwa zaidi.

Hivi karibuni zilisika habari za janga la njaa kuwakumba watu wa Kisiwa cha Pemba na zaidi katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini.

Ili kuupata ukweli, badala ya kutegemea maneno ya mitaani, waandishi wa habari wa vyombo visivyokuwa vya serikali kutoka Unguja, walikwenda Pemba. Vyombo vya habari vya serikali havikuwa na habari yoyote juu ya suala hili kwa vile vina jukumu kubwa la kutoa hotuba za viongozi na msafara wa mbio za Mwenge.

Utafiti wa waandishi uligundua kuwa, katika baaadhi ya vijiji, watu walikuwa wanachimba mizizi ya chochoni, vivu, pata na nondoo ambayo huichemsha na kula ili kuganga njaa kali inayowakibili. Waliwaona watu wakiwa katika hali mbaya, wakiwa wamerembuka na baaadhi ya watu wazima wakiwa wamefunga mikaja kupunguza makali ya njaa.

Hali waliyoikuta ilikuwa ya kusikitisha na kutisha. Lakini, mara tu habari hizo zilipotoka, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kisiwani Pemba, walikuja juu kama vile waandishi wamefanya kosa la uhaini. Polisi wakatumwa kuwakamata na kuwasaili, na maofisa wa Usalama wa Taifa wakawa katika shughuli kubwa, kana kwamba waandishi hao wamevujisha siri muhimu ya serikali.

Tafsiri unayoipata hapa, ni kuwa viongozi wa SMZ hawataki kusikia habari za mambo hadharani. Wao wanataka hata habari za njaa kisiwani Pemba ziwe siri, huku mamia ya watu, wakiwamo watoto wadogo wakiteseka na maisha yao kuwa hatarini.

Kilichogundulika ni kuwa watu katika baadhi ya vijiji vya Micheweni wanahitaji msaada wa haraka wa chakula baada ya mashamba yao ya uwele, mtama na mazao mengine kuathirika vibaya sana na ukame, huku wakiwa hawana akiba ya chakula.

Serikali si ya kulaumiwa kwa janga hili, lakini kitendo cha kutaka kuficha habari hizi ndicho kinachozusha masuala na watu kuuliza: Kwa nini?

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, hakufurahishwa na taarifa za waandishi na amesema hakuna njaa Pemba na labda Wapemba wa Micheweni wameamua kuchimba mizizi na kula kwa kuamini inawasaidia kuwapa nguvu.

Je, mkuu wa mkoa anataka kutuambia ndiyo sasa watu wa Pemba wamegundua kuwa wanayo viagra asilia, na hata kuona ni vyema wawaanzishe na watoto wao kuitumia ili wakiwa wakubwa wawe wamebobea kwa ngono?

Tuache mzaha na tusiingize siasa au utani wa aina yoyote katika suala hili. Njaa haitaki utani na mwenye njaa ni mtu wa kumuonea huruma na kama hutaki kumsaidia, si vizuri kumfanyia kejeli au kebehi.

Ukifanya utafiti wa haraka haraka, utaona baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika wamejenga utamaduni wa kupenda kuficha ukweli, hata wakielewa wakifanya hivyo madhara yake ni makubwa.

Kwa zaidi ya miezi sita katika mwaka 1984, Serikali ya Ethiopia ya dikteta Mengistu Haile Mariam, ilificha habari za maelfu ya watu kufa Ethiopia kutokana na janga la njaa mpaka mpiga picha maarufu wa Kenya, marehemu Mohammed Amin, alipofika katika vijiji vya Ethiopia kwa siri na kuuonyesha ulimwengu hali halisi.

Hapo ndipo nchi mbalimbali zilipopeleka msaada na hata wanamuziki maarufu wa kila pembe ya dunia wakakusanyika na kuimba pamoja ule wimbo maarufu wa “We are the World (Sisi ndio ulimwengu) ili kuchangisha fedha za kuwasaidia waliokumbwa na janga la njaa nchini Ethiopia.

Dunia hii pia imeshuhudia kejeli za aina yake za watu matajiri na wenye vyeo kuwafanyia watu wenye njaa. Mfano mmoja ni wa Imelda Marcos, mke wa aliyekuwa Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos, aliposema alishangazwa kuona maelfu ya watu katika nchi hiyo wakiandamana kulalamika kwamba wana njaa baada ya bei za vyakula na zaidi ya mkate kupanda.

Mama huyu, aliyekuwa na vidani zaidi ya 100 vya dhahabu na almasi na jozi 3,000 za viatu, kwa jeuri na kiburi, alikwenda kwenye kituo cha televisheni na kuwaambia Wafilipino kuwa kama hawawezi kumudu kununua mkate, basi wale keki. Hii ni sawa na kumwambia asiyemudu kununua dagaa anunue kuku.

Inasikitisha kusikia baadhi ya viongozi wa SMZ wanasema tatizo si chakula bali uwezo mdogo wa kifedha wa watu wa Micheweni. Hii nayo ni lugha ya kejeli, jeuri na kiburi.

Hapa watu maskini wanapozungumzia kuwa hawana chakula wanakusudia vyakula wanavyotumia kama mtama, uwele, muhogo, mahindi na viazi vitamu na si vile vinavyopatikana madukani kama mchele, biskuti, chokoleti, siagi au nyama na samaki katika mikebe.

Hawa watu maskini hata wanapozungumzia matibabu, hukusudia yale ya zahanati za vijijini kwao na si yale ya Uingereza, Marekani, Uswisi au India wanayoyajua viongozi wetu na matajiri wa nchi hii.

Kama wapo viongozi wachache hawautaki ukweli juu ya janga la njaa lililopo Pemba, serikali iachane na jeuri yao na maradhi yao ya kukataa kuweka mambo hadharani. Hili si suala la kisisia, na kuligeuza hivyo ni kutaka kupotosha ukweli.

Hivi sasa tunaambiwa serikali inafanya uchunguzi, lakini ieleweke huu uchunguzi hauna maana, kwa sababu kauli za wana vijiji, picha na kanda za video zilizochukuliwa Micheweni zinaonyesha kuwa janga la njaa limevikumba vijiji kadhaa. Picha zinaonyesha watoto wamerembuka na kudhoofika kwa kukosa chakula na si kwa kula hiyo ambayo mkuu wa mkoa anataka tuione kama Pemba Viagra.

Serikali si ya kulaumiwa kwa janga hili lililotokana na ukame, lakini inawajibika kuwasaidia wananchi, pale hali kama hii inapotokea, hata ikiwa imetokana na wananchi kutochukua tahadhari za kujiwekea akiba ya chakula.

Watu wenye uwezo ambao mara kwa mara huchangia shughuli za michezo na burudani watafanya jambo la busara, kama watawasaidia ndugu zetu hawa wanaokabiliwa na njaa. Taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojikita kufanya makongamano na semina katika hoteli za kitalii na kugawa posho kwa washiriki ziachane hivi sasa na mikutano yao na zisaidie watu wa Micheweni.

Vyama vya siasa navyo havina budi kuchangia. Ni lazima vijali maisha ya watu na si kura zao tu wakati wa uchaguzi.

Tushirikiane kunusuru maisha ya watu wa Micheweni wanaokabiliwa na njaa na tuige mfano wa Rais Jakaya Kikwete aliyekataa kuficha habari za watu katika sehemu mbalimbali za Tanzania Bara kukabiliwa na janga la njaa na kuamua kuwapa na kuwaombea msaada.

Hatua za haraka zichukuliwe kabla maafa hayajatukumba na kama ni muhimu kunyoosheana vidole na kupakana matope, hayo yaje baada ya kunusuru maisha ya watu wa Micheweni. Lakini wale wote waliojaribu kuficha ukweli juu ya hali halisi ya Micheweni wawajibishwe. Hatuwezi kuruhusu watu wachache wachezee maisha ya watu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.