SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza viwango vipya vya bei za vyakula ili kukabiliana na mfumko wa bei.
Uamuzi huo umetangazwa jana na Waziri wa Biashara, Utalii na Uwekezaji, Samia Suluhu Hassan, kutokana na kikao cha serikali na wenye kampuni za uingizaji vyakula Zanzibar.
Waziri Samia alisema kwamba kuanzia sasa ni marufuku kwa wafanyabiashara wa mchele, unga wa ngano na sukari kuuza bidhaa hizo bila kuzingatia viwango vya bei vya serikali.
Alisema kwamba wanachukua uamuzi huo baada ya kuafikiana na wafanyabiashara hao, kwamba kodi ya forodha itapunguzwa kwa asilimia 25, ili nao waweze kuwauzia wananchi kwa unafuu.
“Kuanzia sasa, mchele utauzwa kilo moja sh 600, badala ya sh 700, sukari sh 1,050 badala ya sh 1,000, unga wa ngano sh 600 badala ya sh 700,” alisema Waziri Samia.
Alisema kwamba mchele wenye chenga nyingi utauzwa sh 500, lakini hakusema mchele wa Mbeya wala ule mwembamba kutoka India (Basmat) utauzwa kwa sh ngapi.
“Watakaokwenda kinyume na viwango hivi vya bei, watakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisemaWaziri Samia.
Alieleza kwamba Waziri wa Biashara amepewa mamlaka, kwa mujibu wa sheria namba 2 ya 1995, kupanga viwango vya bei kulingana na mwenendo wa soko la dunia.
Alisema kwamba, katika kikao hicho wafanyabiashara wamekubali kupunguza viwango vya faida kwa asilimia 10, kutokana na serikali kuwapatia msamaha wa kodi ya asilimia 25 kwa bidhaa hizo za vyakula.
Hii ni mara ya kwanza serikali kutangaza viwango vya bei za bidhaa za vyakula, tangu kuruhusu mfumo wa soko huria la biashara.
Waziri Samia, alisema viwango hivyo vya bei vitakuwa vikipitiwa kila baada ya miezi miwili, ili kuangalia mabadiliko ya soko la dunia na gharama za ununuaji na usafirishaji.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwenyekti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima, Abdallah Abbas, alisema hatua hiyo itawasaidia wafanyabiashara wa Zanzibar na wananchi.
Hata hivyo, alisema uchakavu wa Bandari ya Zanzibar umekuwa ukisababisha kero kwa wafanyabiashara, kwa vile mizigo mingi huchelewa kutolewa na hivyo kusababisha gharama kuongezeka.
Mwenyekiti huyo alisema kitendo cha serikali kukaa na wafanyabiashara na kuwapunguzia kodi kwa asilimia 25 katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, kitaleta unafuu wa upatikanaji bidhaa kwa wananchi, wakiwamo wale wa vijijini.