WANAFUNZI wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jana waliendeleza mgomo wa kutoingia darasani kwa kuandamana katika eneo la shule na kufikia hatua ya kuwazuia walimu wao kuingia madarasani kufundisha.
Mgomo huo ulianza saa 3.00 asubuhi kwa wanafunzi hao kujipanga barabarani kwa muda wa saa mbili ili kuzuia magari kupita na kuhakikisha hakuna mwalimu anayeingia darasani kufundisha.
Maandamano hayo yaliambatana na nyimbo za kusisitiza madai yao ya kupatiwa ufumbuzi kuhusu mikopo wakati wanafunzi wa mwaka wa kwanza, waliopata daraja la kwanza walihoji uhalali wa kupewa mikopo wakati wana sifa ya kusomeshwa na serikali.
Katika maandamano hayo, wanafunzi hao wanadai kupunguziwa nauli za usafiri, kushushiwa bei ya vyakula katika migahawa yao na kushushiwa bei ya malazi.
Pia wanalalamikia mazingira mabovu wanayosomea, ikiwa ni pamoja na kuwa na vyoo vichafu, mazingira machafu ya kuishi na kuomba uongozi wa Bodi ya Mikopo kuwalipia fedha kwa ajili ya kufanyia usafi.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Nimrod Mkono, aliwaambia waandishi wa habari juzi ofisini kwake kuwa, mikopo ya wanafunzi hao ilichelewa kwa sababu maalumu na tayari walijulishwa sababu za kucheleweshewa.
Mmoja wa wanafunzi ambao aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema wapo baadhi ya wanafunzi wa mwaka huu, ambao tayari wameshapatiwa mikopo hiyo, lakini masharti ya mkopo huo hayaridhishi kwani walistahili kusomeshwa na serikali na si kwa mkopo.
Rais wa wanafunzi hao chuoni hapo, Mwita Magesa, aliiambia Tanzania Daima jana kuwa, angetolea ufafanuzi suala la mgomo wa jana kwani alikuwa wizarani kuwasiliana na wahusika ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mgomo wa wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza waliotaka kuandamana hadi katika ofisi ya Bodi ya Mikopo, ulianza Septemba 15 wakipinga kucheleweshewa mikopo yao. Maandamano hayo hata hivyo yalitawanywa na polisi kwa vile hayakuwa na kibali.