MOTO aliouwasha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wa kuzidodosa hadi kuzikataa taarifa za wakuu wa wilaya (ma DC) wa Mkoa wa Kigoma, umesababisha wakuu wa wilaya wa Mkoa wa Iringa kujawa hofu.
Ma DC hao wana hofu kwa sababu, Waziri Lowassa anatarajia kufanya ziara hivi karibuni mkoani Iringa, na ameshatahadharisha kwamba hataki ripoti za ubabaishaji wala zisizotosheleza, bali anataka zinazokwenda na wakati.
Hofu hiyo imewafanya baadhi ya wakuu wa wilaya wa mkoa huo kukosa usingizi, wakiandaa taarifa zao kwa makini zaidi kwa hofu ya kukumbwa kilichowapata wenzao wa Mkoa wa Kigoma wakati Waziri Lowassa alipokuwa kwenye ziara ya siku tano.
Wapo Ma DC wa Mkoa wa Iringa wanaodaiwa kuchana taarifa walizokwishaziandaa, baada ya kubaini upungufu, hasa baada ya kusikia joto ya jiwe iliyowakuta wenzao wa Kigoma ambao walifikia kushushuliwa mbele ya watendaji wao.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, John Mongella ambaye ni DC wa kwanza taarifa yake kukataliwa hadharani na Waziri Mkuu, aliiambia Tanzania Daima mjini Kigoma kuwa baada ya taarifa ya vyombo vya habari kwamba taarifa yake imekataliwa na Waziri Mkuu, amepigiwa simu nyingi kutoka kwa Ma DC wenzake wakimpa pole, lakini zaidi ya kutoa pole, wanataka wajue upungufu wa taarifa yake ili waandae taarifa zao vizuri.
“Nimepigiwa simu nyingi sana kutoka kwa Ma DC wenzangu wa Iringa na sehemu nyingine nchini, wakitaka kujua waandae vipi taarifa zao ili kukwepa yaliyonikuta.
“Kukataliwa kwa taarifa yangu nimepokea kama changamoto, hasa ukizingatia kuwa ni mara yangu ya kwanza kushika nafasi hii na ni taarifa yangu ya kwanza kama kiongozi wa nafasi hiyo. Kwa kifupi hatua hiyo imenipa ujasiri na changamoto kubwa katika kukabiliana na majukumu yangu,” alisema Mongella.
Wakati wa ziara yake mkoani Kigoma, Waziri Lowassa kwa mara ya kwanza, aliikataa taarifa ya DC Mongella na kuamuru maofisa wake waingie kwenye magari ili kuendelea na ziara badala ya kusikiliza taarifa hiyo kwa maelezo kuwa ilipitwa na wakati.
Mbali ya DC Mongella, Lowassa pia alimpa wakati mgumu DC wa Wilaya ya Kibondo, Luteni Kanali John Mzurikwao kwa kumwambia kuwa taarifa yake ilijaa nadharia na porojo kuliko utekelezaji.
Waziri Lowassa alimpasha DC huyo mbele ya watendaji wake kuwa hajaelewa maagizo ya semina elekezi iliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.
Hata Waziri Lowassa alipojaribu kudodosa kwa kuuliza maswali, DC huyo na watendaji wake walishindwa kabisa kujibu maswali yaliyotokana na taarifa hiyo.
Moto huo hakuuishia kwa Ma DC tu, kwani hata Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Joseph Simbakalia, alikumbana na hali hiyo wakati akitoa taarifa ya mkoa kwa Waziri Mkuu.
Simbakalia ambaye naye ni mgeni katika nafasi hiyo, alikuwa na wakati mgumu wa kujibu maswali mbalimbali ya Waziri Mkuu, baada ya kutoridhishwa na taarifa yake, hasa katika hatua za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo ambao uko nyuma kimaendeleo. Kabla ya kushika nafasi hiyo, Kanali Simbakalia alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Wakati akitoa majumuisho ya ziara yake mkoani Kigoma, Waziri Mkuu aliwaonya ma DC wa wilaya nyingine, ambako atafanya ziara, kuandaa taarifa za maana na zinazolingana na maagizo ya semina elekezi ya Ngurdoto.
“Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Waziri Mkuu anawakosesha usingizi ma DC, ni kweli, lakini nimewasamehe kwa kuwa wengi ni wageni, lakini wengine nitawakosesha kazi baada ya kushauriana na Rais. DC huwezi kusoma taarifa eti Kibondo iko wapi, Magharibi inapakana na nani, hayo mambo nayajua tangu shuleni, nataka kujua mkakati unaotekelezeka, hasa katika suala la elimu, afya na kilimo,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu wiki hii anatarajia kuanza ziara yake mkoani Iringa, hivyo wakuu wa wilaya za mkoa huo watakuwa makini zaidi katika kuandaa taarifa zao ili kukwepa kushushuliwa kama wenzao wa Kigoma.