WATAALAMU wa kilimo nchini, wameshauriwa kutumia utaalamu wao ili kuboresha sekta ya kilimo, na hivyo kuliondolea taifa aibu ya upungufu wa chakula.
Ushauri huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, wakati wa sherehe za uzinduzi wa chama cha wataalamu wa kilimo Tanzania (TSAEE), Kanda ya Magharibi, zilizofanyika katika ukumbi wa NSSF mjini hapa.
Alisema wataalamu hawana budi kutumia ujuzi walionao kwa kufundisha na kueleza umuhimu kwa wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora na kuongeza kuwa wao ndiyo chachu ya kweli katika kuboresha kilimo na hatimaye kumuwezesha mkulima kunufaika na kilimo cha kisasa.
“Kilimo chetu kwa sasa hakitofautiani na kile cha enzi za Adam na Eva, aina hii ya kilimo haiwezi kumkomboa mkulima, ni vema mkatumia utaalamu wenu kuleta mapinduzi ya kilimo ili mkulima ajisikie fahari ya kuitwa mkulima,” alisisitiza Mzuzuri.
Alisema tofauti na wataalamu wa taaluma zingine nchini, baadhi ya wataalamu wa kilimo wamekuwa na tabia ya kutohisi uchungu kuona hali ya kilimo inaendelea kudorora, na hivyo kukifananisha kitendo hicho sawa na ujambazi wa kutumia silaha kwani wanashindwa kuitetea taaluma yao kwa vitendo.
Aidha, mkuu huyo alisema tayari serikali imepanga mikakati endelevu ya kuwasaidia fedha wataalamu wa kilimo ili kukiboresha kilimo nchini.