MBUNGE wa Namtumbo, Vita Kawawa, ametoa rai kwa wakulima nchini kuuza mazao yao kwa kutumia vipimo mizani badala ya kutumia vipimo visivyo halali.
Kawawa alisema wakulima wakitumia vipimo halali, watapata faida badala ya kuendelea kunyonywa kwa kuuza mazao kwa walanguzi kwa kutumia kipimo cha ‘dumla’.
Alisema hayo hivi karibunii wakati wa majumuisho ya ziara ya kulitembelea jimbo hilo katika Kata ya Namtumbo kwa lengo la kuwashukuru wapiga kura.
“Acheni kuuza mazao yenu kiholela, mkubaliane kuuza mazao kwa pamoja ili mpate bei nzuri, tena mpime kwa mizani ili walanguzi wasiendelee kuwanyonya, vinginevyo mtaendelea kunyonywa,” alisema Kawawa.
Akizungumzia zao la tumbaku, mbunge huyo aliwataka viongozi wa vyama vya ushirika kuangalia mikataba wanayowekeana na kampuni za tumbaku, na iwapo mkataba haueleweki, wawaombe wanasheria wa serikali na halmashauri ili mikataba hiyo iwe na manufaa kwa wakulima.
Kuhusu usambazaji wa mbolea ya ruzuku katika maeneo ya vijijini katika msimu
uliopita, Kawawa alisema baadhi ya mawakala hawakuwa waaminifu baada ya kupata kibali cha kusambaza mbolea, waliuza kwa bei ya ulanguzi na kupeleka mifuko michache ya mbolea katika maeneo waliyopangiwa.
Alitoa wito kwa viongozi wa vijiji katika msimu huu wa kilimo, kuhakikisha mawakala wanafikisha kiasi chote cha mbolea walichopangiwa kulingana na kibali walichopewa ili wakulima wasiendelee kuuziwa mbolea ya ruzuku kwa bei kubwa.