HOSPITALI ya rufani ya KCMC ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro iko katika hatua za awali zitakazoiwezesha kuanza kutoa huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Huduma hiyo hivi sasa hufanyika katika Nchi za Ulaya na Asia hususani katika nchi ya India ambako mamia ya Watanzania wenye matatizo ya moyo hulazimika kwenda kupatiwa tiba.
Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya moyo katika hospitali ya KCMC, Profesa Samwel Chughulu, alisema hospitali hiyo kwa sasa iko katika awamu ya nne ya majaribio ya upasuaji unaohusisha kutoa moyo nje ya sehemu yake na kuufanyia upasuaji.
Alizitaja baadhi ya hatua zinazochukuliwa kuwa ni pamoja na kupeleka madaktari na wauguzi wa idara mbalimbali kupata masomo ya juu zaidi, ujenzi wa jengo la kisasa na kupata vifaa vya kisasa zaidi vinavyohitajika kwenye aina hiyo ya upasuaji.
Naye Dk. Duane Cook anayeongoza jopo la wataalamu wa upasuaji huo kutoka Florida, Marekani amesema magonjwa ya moyo yanayohitaji upasuaji mkubwa yanaongezeka katika nchi zinazoendelea na kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho huenda kukawa faraja kubwa kwa Tanzania na nchi jirani.
Alisema pamoja na kuwepo na upasuaji mdogo wa moyo katika nchi za Afrika kusini na Misri ni maeneo mawili tu ambayo bado hayajatosheleza mahitaji ya wanaohitaji huduma hiyo kwa bara zima la Afrika.
Aliongeza kuwa nia ya wataalamu na wadau wengine kutoka nje ni kusaidia Afrika Mashariki kwa kutumia raslimali walizonazo, ikiwemo ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kujenga kitengo kinachojitegemea cha moyo katika hospitali ya KCMC
Baadhi ya wagonjwa waliowahi kufanyiwa upasuaji katika awamu zilizopita Emanuel Isula mkazi wa Morogoro, Godwin Kaaya kutoka Arusha na Catherine Shine kutoka wilayani Rombo mkoani hapa, wameeleza furaha yao baada ya kupata tiba katika hospitali hiyo, kuwa imesaidia na kuwezesha kuwapunguzia gharama iwapo wangepelekwa India kupatiwa tiba ya ugonjwa wa moyo uliokuwa ukiwasumbua.
Upasuaji wa wazi wa moyo ulifanyika katika hatua za majaribio hospitalini KCMC, zimepelekea zaidi ya wagonjwa 30 kufanyiwa upasuaji huo tangu uanze Septemba 2004, ukiongozwa na jopo la wataalamu wapatao 35 kutoka Marekani na hospitali ya KCMC.
Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19318
Na Rodrick Makundi, Moshi