Na Mwandishi wa HabariTanzania.com, Canada
Tarehe 15 Septemba dunia ilizizima hasa ile ya kiislamu. Ilizizima kwa hasira na jazba baada ya kiongozi wa kanisa la kikatoliki la Roma, Papa Bendikto wa kumi na sita, kunukuu maneno ya mtawala kwa kikiristo wa karne ya nne. Mtawala yule alisema nionyeshe jpya aliloleta Mohamad zaidi ya mauaji, ukatili na kueneza dini kwa upanga.
Papa alinukuu maneno hayo alipokuwa ziarani nchini mwake wiki moja kabla ya sakata hili. Alikuwa akitoa mhadhara kwenye chuo kikuu kimoja nchini humo.
Kimsingi Papa hakuwa na nia mbaya ingawa maneno yake yalichukuliwa vibaya kama alivyoomba msamaha siku iliyofuata.
Alichosahau Papa ni kwamba hata yeye nyumba yake si salama linapokuja suala la ni dini gani ilienezwa kwa ukatili na mauji.
Uislam na ukristo kadhali vilienezwa kwa mauaji,vita,unyonyaji hata udhalilishaji.
Hivyo basi hata hao waislamu walioudhiwa na kauli iliyonukuliwa inabidi kwanza waelewe kuwa hawawezi kuandika upya historia na pili wajue wazi kuwa pamoja na dini kuhubiri upendo na mengineyo,dunia inajua kuwa chimbuko la dini zote za kimamboleo ni baya tu.
Wale wanaokumbuka kwa mfano madhara ya utumwa,watakubaliana nasi kuwa walioendesha biashara hii haramu ni waarabu na wazungu.
Pia wakirejea vita kama vile Badr utekaji wa ulaya uliofanya na Othman, wataficha nyuso zao kwa aibu kama kweli chanzo cha maandamano yaliyoshuhudiwa huko India,Pakstani,Palestina ambako tunaambiwa makanisa mawili yalishambuliwa kwa risasa, Iran na kwingineko.
Nani asiyejua kuwa baadhi ya amri kama vile kupiga watu mawe,kuwakata mikono,kuwatenga wanawake, kuwaua murtadi n.k ni ukatili tu?
Kimsingi kwa mfano ukichukua viwango na tafsiri za haki za binadamu za dunia ya sasa,mafundisho yote ya torati ya Musa ni ukatili na unyama usio na ulazima wala yasiyofaa kwa wakati huu. Ni mambo yaliyopitwa na wakati ambayo yalilenga kuwastaarabisha walawi.
Sasa hebu tuangalie Papa amesimama wapi kuhusiana na historia ya kanisa lake. Kuna uwezekano kuwa Papa bila kujua alijikuta kwenye kile waswahili husema nyani haoni nonihino lake.
Kwanza nani asiyejua kuwa mzizi na chanzo cha ukiristo ni umwagaji damu ulioanzia Golgota. Nani hashangai jinsi wakristo wanavyoendelea kutumikishwa chini ya ushirikina wa kisasa ambao hadi tunaandika dunia imeufumbia macho. Hivi nani aweza kula nyama ya mpendwa wake na kumalizia kwa damu yake hata kama ni kwa mfano?
Hili lingefanywa na dini za kiafrika lingeandikwa dunaia nzima na kusema waswahili wanakula nyama za watu yaani cannibalism.
Tutatoa historia kidogo tu ya karne ya kumi na moja juu ya mauaji yaliyofanywa na kanisa la Roma analoliongoza Papa Bendikto.
Mnamo mwaka 1252, Papa Innocent IV alitoa tamko la kipapa lililojulikana kama Ad exstipada. Tamko hili lilielekeza manyanga au na mawakala wa kanisa kuwaua wapinzani wa wakati huo yaani waprotestanti ambao liliwaita heretics. Katika kutekeleza tamko hili la kiuaji mauji makubwa kwa njia za kinyama zaidi yalifanyika. Maana watu walichomwa moto,kuvuliwa nguo,kungolewa macho na mengine kama hayo.
Hiyo haikutosha. Kwani mwaka Ad exstripada iliendelea kupewa baraka na mapapa waliofuata baada ya Papa Innocent.
Alexander IV (1254-61; Clemence IV (1265-68); Nicholaus IV (1288-92) Bonephace VIII (1294-1303) na wengine waliendelea kukazania kutumika kwa tamko hili chafu la kipapa.
Katika ngwe ya pili ya mauaji haya watu walikatwa nyayo, walichomwa kwa vyuma vya moto sehemu nyeti za mwili,kunwagiwa maji ya baridi na njia nyingine za kinyama na utesaji mkubwa ambao binadamu hakuwahi kuushuhudia.
Katika unyama huu historia inasema kuna vitu vilivyotumika kama Iron virgin na Spanish boots haviwezi kusahaulika.
Kwa wale watakaotaka rejea tunawashauri wasome, Redpath’s history of the world. Hebu turejee kutoa baadhi ya visa vya mauaji yaliyofanywa na kanisa vilivyoitingisha historia ya mwanadamu.
Francis Gamba (1554) alipopinga mauaji yaliyondeshwa na kanisa alilazimishwa kutubu na kufuta maneno yake. Alipokataa alinyofolewa ulimi maskini. Waliokuwa na mawazo kama yake walichomwa kwa kumwagia chuma cha moto, molten kwenye matundu ya macho na masikio. Papa inabidi ajitahidi kusoma historia ili asijikwae bure hata kama nia yake siyo kuwashutumu wenzake.
Mwaka 1209 mji wa Beziers ulivamiwa na mawakala wa Papa ambapo watu wapatao 60,000 waliuawa kinyama.
Hii haikutosha.
Mwaka 1211 Gavana wa Lavaur alinyongwa huku mkewe akifungiwa jiwe na kuzamishwa kwa kosa la kupingana na amri ya kanisa ya kuwaua wapinzani wapatao 100,000. Hawa walijulikana kama Albigenses au waprotestanti.
Mwaka 1562 chini ya amri ya Papa Pius IV mauaji maarufu ya Orange yalifanyika ambapo wahanga walichinjwa na kudhalilishwa vibaya sana.
Mwaka 1572 Huguenots au waprotestanti kama walivyojulikana kipindi hiki waliuawa.
Baada ya mauaji haya yalifuatia mauaji ya Paris ambapo Papa Grigory XIII aliadhimisha misa ya kumshukuru Mungu kwa mauaji haya kwenye kanisa la Mt. Barthromeo.
Kwa furaha ya ukumbusho wa matukio hayo ya Orange na Paris ilitengenezwa sarafu iliyobeba picha ya Malaika akiwa ameshika panga mkono mmoja kuwamaliza wapinzani na msalaba mkono wa pili kuuimarisha ukristo.
Sarafu hiyo ilibeba maneno "ugonottorum stranges 1572.
Kwa uchache huo ndiyo ushahidi wa kuonyesha kuwa nyumba ya papa siyo safi. Tunaamini kuwa alilijua hili. Kama lengo la Papa kama ilivyokuwa azma yake ya mwanzo ni kuleta usuluhisho wa kiimani, hakufanya kosa kurejea historia maana siku zote kusuluhisha ni kama kufanya kesi mahakamani ambapo matukio hurejerewa.
Kwa bahati mbaya waislam kwa vile wameishajenga dhana kuwa dunia haiwapendi hasa baada ya dini hii kuhusishwa na ugaidi, walielewa ndiyo siyo.
Pia kuna haja ya dunia kuanza kutafuta jinsi ya kushughulikia tabia mbaya inayoanza kujitokeza ambapo watu chini ya kisingizio cha dini yao wanataka wasisemwe wala kuambiwa ukweli.
Tabia hii bila shaka ndiyo mama wa uhafidhina unaoisumbua dunia iwe ni kutoka kwa waislamu au wakristo.
Kimsingi somo tunalolipata ni utukufu wa dini zetu za kiasili ambazo hazina historia ya uchafu,uongo,udhalilishaji wala mauji kama dini hizi mbili za kikoloni ambazo zimeanza kuwa kero na tishio la usalama wa wale tusioziamini.
Bahati mbaya dini hizi zimeanza kujijengea uhalali kiasi cha kutishia mstakabali mzima wa dunia.
Kimsingi kilichosemwa na Papa hakikuwa kipya wala kibaya bali kurejea historia. Kama kungekuwa na nia mbaya basi Papa angekuwa sawa na kasa anayemcheka kobe au ng’ombe anayemcheka nyati. Kwani dini zote zina damu na dhambi nyingi mikononi mwake.