Licha ya jiji la mwanza kuwa la kwanza kitaifa katika usafi wa mazingira, shirika moja la mazingira limedai kuwa bado viwanda vilivyoko mwanza vinachangia kuharibika kwa mazingira na uchafuzi wa maji ya ziwa Victoria.
Katibu mkuu wa shirika la mazingira mkoani mwanza Mwanza Environmental Sympayhiser- MES Bw. Kissussi Bolinga akiongea na waandishi wa habari za mazingira jijini hapa ameeleza kuwa viwanda vingi vilijengwa bila kuzingatia hifadhi ya mazingira.
Amefafanua kuwa maji machafu yanayozalishwa na viwanda hivyo hayakuelekezwa wapi pa kwenda bila kuathiri mazingira na badala yake humwagwa katika ziwa Victoria na na hivyo kuhatarisha usalama wa viumbe vya ndani na nje ya ziwa hilo.
Bw. Kissussi amebainisha kuwa viwanda kama Vickfish, Tanpich, TBL, Cocacola na Mwatex vyote havina miundo mbinu sahihi ya kusafisha maji machafu kabla ya kuyarejesha katika ziwa.
Aidha Bw. Kisussi amewapongeza wakazi wa jiji la Mwanza kwa jitihada zao za kusafisa mazingira ingawa amekiri kuwepo kwa mipango mibaya ya jiji ambapo watu wengi waishio milimani huishi chini ya viwango vya kiafya.
Amebainisha kuwa wakazi wa milimani wengi wao wamejenga nyumba zao bila ramani na katika viwanja visivyopimwa na kwamba hawana vyoo vinavyokubalika kiafafya na hivyo kuchangia kuwepo kwa uchafu katika jiji la mwanza.
Afisa mtendaji wa Kata ya Igogo jijini ambapo watu wengi wamejenga kihorela katika milima Bw. Moris Maduhu alipohojiwa juu ya usafi kwa wanaoishi milimani katika kata yake alikiri kuwa wengi hawana vyoo na kwamba hali hiyo inatokana na uzembe wa viongozi kutowabana.
Bw. Maduhu amesisitiza kuwa kutokuwepo kwa vyoo kunatokana na mwamko wa wakzi wa milimani, kukosa nafasi ya kuchimba vyoo kutokana na msongamano wa majumba pamoja na maeneo hayo kuwa na mawe mengi yanayozuia juhudi za uchimbaji wa vyoo kwa wasio na uwezo kiuchumi.
Uchunguzi uliofanywa na wanamazingira umebaini kuwa wakazi wengi wa mkoa wa mwanza hawana utamaduni wa kuwa na vyoo hali inayopelekea wengi wao kujengewa vyoo vyao na mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayotoa huduma jijini mwanza.